Tanzania yazisaidia nchi zilizokumbwa na kimbunga

20Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Tanzania yazisaidia nchi zilizokumbwa na kimbunga

TANZANIA imetoa msaada wa dawa, chakula na vifaa vya kujihifadhi kwa Msumbiji, Malawi na Zimbabwe ili kuwasaidia waathirika wa kimbunga cha Idai kilichosababisha mafuriko yaliyozikumba nchi hizo wiki iliyopita.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi (wa tano kulia) na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, wakibabidhi misaada ya dawa na vyakula, jijini Dar es Salaam jana, ambavyo serikali ya Tanzania imetoa kwa nchi za Malawi, Msumbiji na Zimbabwe, ambazo zimekumbwa na maafa ya mafuriko kufuatia tufani kali iliyolikumba eneo hilo la kusini mwa Afrika. PICHA: SULTANI KIPINGO

Msaada huo ulikabidhiwa jana kwa mabalozi wa nchi hizo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, sehemu ya msaada huo kwenda nchi za Zimbabwe na Msumbiji ikisafirishwa jana kwa kutumia ndege za Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ).

Akizungumza wakati wa kupakia msaada huo kwenye ndege ya jeshi hilo, Prof. Kabudi alisema Rais John Magufuli ameagiza kutolewa kwa msaada huo na kutoa salamu za pole kwa marais wa nchi zilizokumbwa na kimbunga hicho.

"Mheshimiwa Rais Magufuli baada ya kupata taarifa hizi na kuzungumza na marais wenzake wa Msumbiji, Malawi na Zimbabwe, Tanzania imeona ni vyema kutokana na undugu wetu, umoja wetu na ujirani wetu, tuweze kuwapelekea msaada angalau kidogo wa dawa na chakula na pia kuwapa pole kwa maafa haya makubwa yaliyowapata," Prof. Kabudi alisema.

Waziri huyo alisema malori saba yenye shehena ya tani 200 za mahindi, yalitarajiwa kuondoka Mbeya jana kwenda Malawi ambako taarifa zilieleza kuwa watu 122 wamepoteza maisha na zaidi ya 1,000 wamekosa mahali pa kuishi.

Alisema tani saba za mchele, dawa na vifaa vya kujihifadhi zitasafirishwa kutoka Dar es Salaam kwa kutumia ndege ya jeshi kwenda Msumbiji ambako taarifa zinasema watu 221 wamefariki dunia na tani nyingine saba za mchele, chakula na vifaa vya kujifadhi vitasafirishwa kutoka Dar es Salaam kwa ndege ya jeshi kwenda Zimbabwe ambako watu 98 wamefariki dunia.

Waziri Mwalimu alisema serikali imetoa tani 24 za dawa, kila nchi ikipatiwa tani nane zinazojumuisha dawa za kuzuia maambukizo ya magonjwa (antibiotics), dawa za magonjwa ya tumbo, dawa za kutuliza maumivu, dripu, shuka, blanketi, magodoro na vyandarua.


Akipokea msaada huo kwa niaba ya nchi yake, Balozi wa Msumbiji nchini, Monica Mussa, alimshukuru Rais Magufuli na Tanzania kwa msaada huo, akieleza kuwa utasaidia kunusuru maisha ya watu wengi ambao hawana chakula na wanahitaji dawa na malazi.

Balozi wa Malawi nchini, Glad Chembe Munthali, pia alimshukuru Rais Magufuli na serikali kwa msaada huo na kueleza kuwa ni wa haraka na umedhihirisha undugu, ujirani na umoja wa dhati uliopo kati ya Tanzania na Malawi.

Kaimu Balozi wa Zimbabwe nchini, Martin Chavenika, mbali na kutoa shukrani zake za dhati, alimhakikishia Rais Magufuli na serikali kwa ujumla kuwa msaada huo utawafikia walengwa.

Mkuu wa Mafunzo na Utendaji Kivita wa Kamandi ya Jeshi la Anga, Brigedia Jenerali Francis Shirima, alisema jeshi litahakikisha msaada wote uliotolewa unafika kwa nchi hizo na kukabidhiwa kwa wahusika.

Habari Kubwa