TARI yawashauri Wakazi wa Kagera kutumia maharage yaliyotafitiwa

28Nov 2021
Lilian Lugakingira
Bukoba
Nipashe Jumapili
TARI yawashauri Wakazi wa Kagera kutumia maharage yaliyotafitiwa

​​​​​​​WAKAZI wa Mkoa wa Kagera wameaswa kutumia maharage yaliyofanyiwa utafiti na kubainika kuwa na madini ya Chuma na Zink, ambayo yanaongeza kinga katika mwili wa binadamu na kusaidia kukabiliana na magonjwa mbalimbali ikiwamo Uviko 19.

Mtafiti wa zao la maharage kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kituo cha Maruku, kilichoko wilayani Bukoba mkoani Kagera, Julius Mbiu, amesema kuwa awali walikuwa na maharage ya JESCA ambayo yana kiwango kikubwa cha madini ya Chuma na Zink, lakini baadae walipata aina nyingine za maharage, ambayo yana kiwango cha juu cha madini hayo zaidi ya JESCA.

"Lakini pia TARI Maruku sasa tumetoa maharage mengine ambayo ni TARIBEAN 2, TARIBEAN 4 na TARIBEAN 5 haya yana kiwango kikubwa zaidi cha madini hayo kuliko JESCA" amesema.

Mbiu amesema kuwa aina hizo za maharage lishe zitasaidia kuboresha afya za wananchi na kupambana na utapiamlo kwa watoto mkoani Kagera.

"Kazi ya madini ya Chuma ni kuongeza wingi wa damu kwenye mwili wa binadamu, kwa hiyo tunawahamasisha wananchi hasa watoto na wanawake kula maharage haya kwa wingi kwa sababu yana madini ya chuma ya kutosha" amesema.

Amesema madini ya Zink yanasaidia katika makuzi ya mfumo wa fahamu kwa mwanadamu, na kuwa pia yanasaidia mfumo wa uzazi wa wanawake na wanaume.

"Badala ya kwenda kuangaika kutumia mbinu nyingine kuimarisha mfumo wa uzazi, wananchi wanapaswa kula maharage haya kwa wingi yatawasaidia kuongeza nguvu kwenye mfumo wao wa uzazi" amesema.

Habari Kubwa