TARURA yarejesha mawasiliano yaliyokatwa na mvua

21May 2020
Dotto Lameck
Babati
Nipashe
TARURA yarejesha mawasiliano yaliyokatwa na mvua

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), imeendelea kurejesha mawasiliano katika maeneo mbalimballi nchini yaliyoathiriwa na mvua ambayo yalikuwa yakisababisha adha kwa watumiaji wa barabara pamoja na madaraja.

Daraja la masware baada ya matengenezo.

Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Mhandisi Said Mikongomi, amesema kuwa tayari wamerejesha mawasiliano katika maeneo mbalimbali na sasa wananchi wanaendelea na shughuli kama kawaida.

‘‘Tumeanza kurejesha mawasiliano katika maeneo mbalimbali ili wananchi waweze kupita na kuendelea na shughuli zao za kiuchumi, maeneo yaliyorekebishwa ni pamoja na daraja la masware ambalo tayari linapitika na daraja hili pia linapitisha malighafi zinazoenda katika kiwanda cha sukari cha Babati’’ amesema Mikongomi.

Daraja la masware kabla ya matengenezo.

mkazi wa Mtaa wa Matufa wilayani hapo, Dominic Mao, amesema kuwa wananchi walipata shida sana kuvuka daraja la Masware baada ya ukuta wa daraja hilo kuanguka lakini kwa sasa tayari ukuta huo umerejeshwa na hivyo wanapita vizuri na kazi zinaendelea kufanyika kwa urahisi.

“Tunawashukuru sana TARURA kurejesha mawasiliano katika daraja hili kwani hili ni daraja la muhimu kwetu kwani tunapitisha mazao lakini pia malighafi zinazopelekwa katika kiwanda cha sukari cha Babati’’ amesema Mao

Habari Kubwa