TAS yatoa vifaa tiba vya milioni 72 kwa wenye ualbino Moro

28May 2020
Christina Haule
MOROGORO
Nipashe
TAS yatoa vifaa tiba vya milioni 72 kwa wenye ualbino Moro

CHAMA cha watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) kimetoa seti tisa za vifaa tiba vyenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 72 kwa watu wenye ualbino kwenye mikoa tisa nchini.

Daktari Wa magonjwa ya ngozi kutoka hospitali ya Rufaa mkoani Morogoro Dk. Janeth Peter (kulia) akimkamulia mkononi tiba maalum ya gesi ya kuua chembechembe za saratani ya ngozi Jamilah Abubakar (35) aliyefika katika ofisi za TAS kupata vifaa tiba. (Picha na Christina Haule, Morogoro)

Akizungumzia hilo Mwenyekiti wa TAS Taifa, Mussa Kabimba, alisema kila mkoa utapewa seti moja ya vifaa hivyo zikiwemo losheni za kujikinga na saratani ya ngozi vyenye jumla ya thamani ya shilingi milioni 8 ambapo wameanza utoaji wa vifaa hivyo katika Manispaa Morogoro.

Alisema upatikanaji wa vifaa hivyo ni juhudi za TAS ambapo wanaiomba Serikali kuona umuhimu wa kuingiza suala la upatikanaji wa vifaa hivyo kwenye sera ili waweze kupata kwa wakati kutokana na kwamba wanaopata ulemavu wa ngozi asilimia 75 wanatoka kwenye familia zenye kipato cha chini hasa maeneo ya vijijini.

Hata hivyo alisema kutokana na uwepo wa Tanzania ya viwanda Serikali ifanye utaratibu wa upatikanaji wawekezaji wa kujenga kiwanda cha mafuta ya ngozi (lotion) hizo ili kuweza kusaidia upatikanaji kwa wepesi lakini pia kuingiza fedha nchini baada ya mafuta hayo kuuzwa nje ya nchi.

“pale ocean road tunahudumia pia na watu wenye ualbino kutoka nchi za jirani kama Congo, Rwanda na Uganda, tukiwa na kiwanda tunaweza kuuza nchi zingine na kukuza uchumi wa nchi pia” alisema Kabimba.

 Alisema upatikanaji wa mafuta na vifaa kinga hivyo utasaidia kupunguza au kuondoa kabisa viashiria vya magonjwa ya saratani ya ngozi kwa watu wenye ualbino na hivyo kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta tiba na wengine kushindwa kufika hospitali maalum kutokana na kukosa nauli.

Kabimba alisema tiba ya Saratani ya Ngozi inapatikana katika hospitali tatu nchini ikiwemo Ocean road, KCMC na Muhimbili ambapo mgonjwa kuweza kufika itamgharimu fedha na muda mwingi na pengine kuishia kupoteza maisha.

Naye Mwenyekiti wa TAS mkoa wa Morogoro Hassan Mikazi aliwataka watu wenye ualbino mkoa wa Morogoro kujitokeza kwa wingi kupata tiba hizo zinazotolewa bure kwenye ofisi za TAS mkoa.

Mikazi alisema, wamelenga kuwafikia watu 100 wanaoishi katika Manispaa ya Morogoro kupata tiba ya uchunguzi wa saratani, kuwapa vifaa kinga mafuta (lotion) na barakoa pamoja na sanitizer kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya Corona.

Naye Daktari wa ngozi kutoka katika hospitali ya Rufaa mkoani Morogoro Dk. Janeth Peter alisema tayari watu 30 wameshapatiwa huduma hiyo kwa siku ya kwanza ambapo watu wawili tu wameonekana wanadalili za viashiria vya saratani ya ngozi katika Manispaa ya Morogoro.

Alisema hujishughulisha na watu hao kwa kuwapa losheni ya kujikinga na mionzi ya jua na mafuta (cream) ya kusaidia ngozi zao kuwa laini, kuwapuliza kwa mashine maalum ya gesi ya kuua vichembechembe vya saratani vilivyoanza sambamba na kupewa elimu ya kutunza ngozi zao kwa kuvaa nguo yenye mikono mirefu na kofia pana inayofunika shingo.

Dk. Peter alisema katika kliniki zao huwafundisha kutambua dalili za awali za saratani ya ngozi ikiwemo kushika ngozi na akiona sehemu ngumu atambue kuwa ni dalili mbaya na ahudhurie kituo cha afya cha karibu nae.

Hata hivyo watu wenye Ualbino waliofika kupata huduma hiyo akiwemo Phabian Nestory (24) mkazi wa Kata ya Sabasaba na Jamila Aboubakar (35) mkazi wa K,ndege Manispaa ya Morogoro kwa nyakati tofauti waliishukuru TAS kwa juhudi wanazoendelea kuzionesha kwao kwa kufanikisha upatikanaji wa vifaa hivyo kila mwaka.

Walisema kwa matumizi ya mafuta ya kupaka usiku na mchana ana imani wanaweza kupambana na saratani ya ngozi ambayo kwao imekuwa tishio.

Hivyo waliiomba Serikali kuweka agenda na kipaumbele katika kundi hilo ili kuwawezesha kupata mafuta hayo kila baada ya miezi mitatu bila wasiwasi kwani ndio kinga kubwa kwao wanayoitegemea katika maisha. 

Habari Kubwa