TASAF yawaokoa wazee waliotelekezewa wajukuu

23Jan 2022
Elizaberth Zaya
Handeni
Nipashe Jumapili
TASAF yawaokoa wazee waliotelekezewa wajukuu

BAADHI ya Wazee waliopo katika Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), wilayani Handeni mkoani Tanga, wamesimulia namna mpango huo ulivyowasaidia kulea wajuu wao waliotelekezewa na watoto wao.

Bibi Amina Mwaliko(64) aliyetelekezewa wajukuu.

Wakizungumza mbele ya Maofisa wa TASAF waliowatembelea, wazee hao walisema baada ya kutelekezewa wajuu waliishi katika maisha magumu ya kuwalea, lakini kwa msaada wa mpango huo, imekuwa rahisi kuwalea na kuwahudumia kwa mahitaji yote ya msingi.

Elizabeth Mganga (70) mkazi wa mtaa wa Kampene katika Kata ya Kidereko, alisema yeye aliachiwa mjuu wake tangu akisoma chekechea akiwa hana uwezo wa kumlea na hivyo wakati mwingine alilazimika kuomba chakula kwa majirani ili wale.

"Mtoto wangu alikuwa ameolewa lakini bahati mbaya akafariki na alikuwa na mtoto mmoja, baada ya hapo familia wakakubaliana kwamba mtoto ataishi na baba yake mzazi kwa sababu mimi sina nguvu za kumtunza, lakini cha kushangaza baba yake alikuja akamtelekeza hapa kwangu na kuondoka zake,"alisema Mganga.

"Nilijua labda atakuwa analeta hata pesa au chakula kwa ajili ya mtoto lakini haikuwa hivyo, kwa hiyo nikawa nahangaika, hata mlo mmoja kwetu ilikuwa ni shida, mara nyingi tulikuwa tunakunywa uji na njaa ikizidi inabidi niende tu kwa majirani niwaombe wanisaidie na ukikuta msamaria mwema anakupatia hata pesa ukanunue chakula hata cha siku mbili, shuleni mtoto wakati mwingine alikuwa haendi kwa sababu ya njaa."

Mganga alisema tangu alipoingizwa katika mpango wa kunusuru kaya masikini, maisha yake yamekuwa bora, anapata milo mitatu kwa siku, na kumtunza mjuu wake ambaye kwa sasa anasoma kidato cha sita na amejenga nyumba ya vyumba viwili baada ya kutunza pesa kidogo kidogo.

"Naishukuru sana TASAF, bila hivyo sijui maisha yangu yangekuwaje, hata hii afya niliyonayo ni kwa sababu mpango huu umeniwezesha nakula vizuri na nalala pazuri,"alisema Mganga.

Amina Mwaliko (64) mkazi wa Msasa Shule, Handeni, alisema yeye alitelekezewa wajukuu sita na hivyo kujikuta akiishi maisha magumu kutokana na kipato chake kuwa kidogo.

"Maisha yangu nilikuwa nayaendesha kwa kutegemea kuuza mboga za majani mitaani na kipindi kile nilikuwa naishi maisha yangu ya kawaida kwa sababu sikuwa na familia kubwa, lakini hali ilianza kuwa ngumu baada ya kutelekezewa wajukuu sita ambao ni wa watoto wangu wawili, hawakuwa wanawajali kwa chochote na hivyo hali ikawa ngumu hata chakula kikawa cha taabu, "alisema Mwaliko.

"TASAF ndio ilikuja kunikomboa kupitia mkutano wa kijiji ambao ndio ulinipendekeza baada ya kuona hali ya maisha niliyokuwa nayo. Huu mpango niliuona kama mkombozi wangu, umenisaidia sana, kwa sasa maisha yangu ni mazuri na kupitia pesa kidogo ninayopewa nimejibana na kuanzisha biashara ndogo na nafuga kuku, tunaishi vizuri,"alisema Mwaliko.

Habari Kubwa