Tatizo la nyonga sasa janga

23Mar 2019
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
Tatizo la nyonga sasa janga

DAKTARI Bingwa wa mifupa, viuno na kikombe cha kiuno katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Edmund Ndalama, amesema tatizo la watu kuvunjika viuno ni kubwa na kwa siku wanawatibu wagonjwa watano.

Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano  kwa ajili ya kupeana uzoefu na wataalamu kutoka India.

Dk. Ndalama alisema kwa mwezi wanatibu wastani wa wagonjwa 20, idadi ambayo ni kubwa ikilinganishwa na nchi zingine.

“Tatizo la kuvunjika kiuno ni kubwa sana na inasababishwa na ajali.  Mtu kuanguka  au mtu akiwa katika shughuli zake za kawaida bahati mbaya anakuwa anakandamizwa yaani kitu kimoja anatembea, kingine kinamkandamiza na anavunjika kiuno,” Dk. Ndalama alisema.

Alisema kuna aina 10 za mivunjiko na kwamba zisipotibiwa mgonjwa atalazimika kwenda kuwekewa kiungo cha bandia.

“Sehemu ya kiuno ni kitu kilichoachwa yaani imesahaulika inahitajika kupewa kipaumbele zaidi unapopata maumivu katika nyonga unaweza ukawa unakufa, huku unaongea ndiyo maana tunawaelimisha watu wajifunze,” alisema.

Alisema mtu aliyepata shida ya nyonga asipotibiwa anapata matatizo makubwa na kushindwa kufanya tendo la ndoa jambo ambalo linaumiza kisaikolojia.

Aidha, alisema wana takwimu ambazo bado hazijachapishwa hivyo kwa sasa wanazifanyia uchambuzi ifikapo Novemba mwaka huu zitatangazwa rasmi.

Naye Daktari Mwandamizi wa Mifupa MOI na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Billy Haonga, alisema kuna mivunjiko ambayo inahatarisha maisha kama hatua za haraka hazijachukuliwa kwa kuwa mgonjwa anaweza kupoteza maisha.

“Kama mvunjiko umeenda kugusa kwenye mshipa mkubwa wa damu hapa hatuna cha kufanya mgonjwa atakufa pale pale alipopatia ajali ndiyo maana unaona mtu kagongwa ghafla anakufa na hata kwenye ajali unaona wengine wanakufa na wengine wanapona,” alisema.

Dk. Haonga alisema wako ambao wanavunjika mishipa midogo midogo ambayo iko katika nyonga. Alisema mtu huyo hujikuta anavuja damu kidogo kidogo, hivyo ana uwezo wa kufika hospitalini na ni lazima kuwapo na huduma ya haraka ili damu isiendelee kutoka.

Alisema mgonjwa wa nyonga kama hajapatiwa huduma ya kwanza anaweza kupoteza maisha, endapo haitaungwa vizuri mwili wake mmoja utakuwa uko juu na mwingine utakuwa chini, hivyo kutembea na maumivu.

“Kwa bahati mbaya matibabu haya yanapatikana Tanzania hapa MOI, hivyo aliyepata ajali mkoani Kigoma asipokuja Dar es Salaam anaweza kubaki na kilema cha maisha au kuwa na mguu mfupi,  mguu usiokuwa na ufahamu na kupata maumivu kutokana na eneo aliloumia kushindwa kuunga,” alisema.

Alisema gharama nyingi ziko kwenye vifaa katika kumtibia mgonjwa na changamoto kubwa ni upatikanaji wa damu wakati wa kumhudumia mgonjwa.

“Ni lazima damu iwapo kwa kuwa inapokosekana unapoteza uhai wa mgonjwa, hivyo kikubwa kinachotuathiri ni upatikanaji wa damu, vile vyuma tunavyowawekea wagonjwa sio gharama kubwa,” alisema.

Habari Kubwa