Tatoa wachangishana kukabili corona mipakani

25Mar 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Tatoa wachangishana kukabili corona mipakani

WANACHAMA wa Chama cha Wamiliki wa Maroli Tanzania (TATOA) kupitia kampuni zao binafsi, wamechangisha vifaa vya kusafisha mikononi maji ya sanitizer kwa ajili ya kusambazwa kwenye maeneo ya mipaka na nchi jirani.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati akikabidhi vifaa hivyo kwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angelina Ngalula, Makamu Mwenyekiti wa Tatoa, Elias Lukumai, amesema Tatoa ambayo ni miongoni mwa kongani 14 za TPSF
wamejitolea kuchangia vifaa hivyo ili kuchangia jitihada za serikali kuzuia maambukizi ya ugonjwa nchini.

“Tumekabidhi vifaa hivi kwa TPSF ili iwezekukabidhi vifaa Ofisi ya Waziri Mkuu mapema wiki ijayo,” alisema Lukumai na kuongeza kuwa wametoa siku tatu zaidi kwa wanachama wao kuendelea kuchangia vifaa hivyo muhimu.

Alisema vifaa hivyo vitasambazwa kwenye maeneo ya mipaka ya Tunduma, Rusumo, Kasumulo na Kabanga na kuwaomba wanachama kuendelea kuonyesha uzalendo na upendo kwa kuchangia vifaa ili visaidie kuzuia maambukizi yasienee zaidi.

“Elimu imeendelea kutolewa kwa madereva wetu wanaosafiri nje ya mipaka umuhimu wa kujikinga na maambukizi ya corona. Hata hivyo, mpaka sasa ninafurahi kusema kuwa hana dereva aliyepata maambukizi,” alisema.

Ngalula mbali ya kuishukuru Tatoa kwa mchango wake wa vifaa, alirudia tena wito wake kwa kongani zingine ndani ya TPSF kuendelea kujichangisha na pia kuiga mfano wa Tatoa.

“TPSF tumejielekeza zaidi katika mambo makuu matatu ambayo ni kutoa elimu zaidi kuhusu maambukizi ya ugonjwa huu kwa muungozo na maelekezo ya serikali kupitia Wizara ya Afya,” alisema.

Alisema wataendelea kuhamasisha zaidi upatikanaji wa rasilimali vitu kutoka kwa wanachama wake ili kuchangia juhudi zinazofanywa na serikali.

Naye Mjumbe wa Tatoa, Saad Ismail, aliwahamasisha wamiliki wa malori kuendelea kuchangia vifaa na kusema kuwa mpaka sasa kuna malori zaidi ya 20,000 ambayo yanafanya kazi.

“Kila mwanachama wa Tatoa ni lazima achukue hatua ya kuchangia kwani janga hili ni kubwa na vizuri tukachukua hatua za kujikinga mapema,” alisema.

Habari Kubwa