TBA yakabidhi jengo jipya Ofisi ya Utumishi

22Mar 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
TBA yakabidhi jengo jipya Ofisi ya Utumishi

OFISI ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora leo imekabidhiwa jengo lake jipya la Wizara katika eneo la Mtumba jijini Dodoma na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

Jengo hilo ni miongoni mwa majengo ya wizara mbalimbali ambayo ujenzi wake ulianza Desemba 4, mwaka jana baada ya Rais John Magufuli kuagiza ujenzi huo.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa jengo hilo, Waziri wa Ofisi hiyo, George Mkuchika amesema kuanzia Aprili 2, mwaka huu ataanza kupatikana kwenye ofisi hizo mpya pamoja na Naibu Waziri na Makatibu wakuu wake.

Amesema anamshukuru kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Magufuli kwa kuwapatia fedha za kuwezesha ujenzi wa ofisi, kupitia ofisi hiyo heshima ya utumishi wa umma itaendelea kupanda na kutaminika zaidi.

“Jengo tunalokabidhiwa leo ni moja tu kati ya mengi kama mlivyoona huko nje, majengo hayo ya ofisi za Wizara na taasisi za serikali yote haya hayaoti tu kama uyogapori, ni kwa jitihada za ufadhili wa serikali ya awamu ya tano kupitia hodi za wananchi kwa Tanzania,” amesema

Amebainisha ofisi yake imejipanga kuwapatia watumishi wote usafiri kila siku kwa ofisi zote mbili za Mtumba na iliyopo Chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM).

Awali,Mkurugenzi wa Idara wa Ujenzi kutoka TBA, Humprey Killo amesema ujenzi wa ofisi hiyo ulianza Desemba 26, mwaka jana na kwa awamu hiyo ya kwanza imegharimu kiasi cha Sh. Milioni 996.

Habari Kubwa