TBA yapania kuondoa wadeni wote sugu

23Mar 2017
Joseph Mwendapole
Dar es Salaam
Nipashe
TBA yapania kuondoa wadeni wote sugu

WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA), imewatahadharisha wapangaji wake kuwa, timua timua ya wapangaji iliyoanzishwa si nguvu ya soda na kwamba wale wote wanaokaidi kulipa kodi ya pango wataondolewa.

Mtendaji Mkuu wa TBA, Mhandisi Elius Mwakalinga.

Mtendaji Mkuu wa TBA, Mhandisi Elius Mwakalinga, alisema hayo jana alipozungumza na Nipashe kuhusu operesheni ya kuwatoa wadaiwa sugu inayoendelea kwenye mikoa mbalimbali nchini, operesheni hiyo inafanywa na kampuni ya udalali ya Yono.

Alisema kuna wapangaji ambao wamekuwa wakichezea mali za umma kwa kukaidi kulipa kodi, lakini alisema muda huo haupo tena kwa kuwa wasiolipa wataondolewa wote.

“Mpaka sasa Yono imefanya kazi nzuri na kubwa na hivi karibuni tutakaa nao tufanye tathmini kujua kazi iliyofanyika na namna ya kusonga mbele kuhakikisha tunamaliza operesheni hii kwa mafanikio makubwa,” alisema Mwakalinga.

Aliwataka pia wadaiwa wote walipe madeni yao na wasijidanganye kwamba huu ni moto wa mabua kwa kuwa wataondolewa mpaka wote waishe.

Mwakalinga alipongeza uaminifu ulioonyeshwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo wanavyoendesha operesheni hiyo na kufanikiwa kuwaondoa wadaiwa sugu bila kujali hadhi na umaarufu wao.

“Yono imefanya kazi nzuri na inaonyesha hawachukui hata rushwa. Mfano mzuri ni pale walipowaondoa wale mapapa wa Dar es Salaam na hiyo haikuwa kazi ndogo,” alisema Mwakalinga.

Mwakalinga alikuwa kampuni maarufu ikiwamo Simon Group imeondolewa kwenye majengo ya TBA maeneo ya Kamata sambamba na Kampuni ya Air Msae iliyokuwa jirani na maeneo hayo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Yono, Scholastica Kevela, alisema operesheni hiyo ni endelevu na kwa wapangaji wengine ambao wanadaiwa na TBA ni vyema walipe madeni yao kabla hawajaondolewa.

“Wanaodhani hii ni nguvu ya soda wanajidanganya maana moto huu hautazimika. Ni vyema wanaodaiwa wajisalimishe kabla hatujawafikia na kuwaondoa kwenye majengo hayo,” alisema.

Habari Kubwa