TBS, ZBS watakiwa kudhibiti njia za panya

22Mar 2019
Joseph Mwendapole
Dar es Salaam
Nipashe
TBS, ZBS watakiwa kudhibiti njia za panya

KAMATI ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, imeishauri Menejimenti ya Shirika la Viwango nchini (TBS), kushirikiana na Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS), ili kudhibiti njia zote za panya zinatotumika kuingiza bidhaa zisizo na ubora.

Wajumbe wa kamati hiyo walitoa ushauri huo juzi, jijini Dar es Salaam, walipotembelea shirika hilo kujionea shughuli mbalimbali za udhibiti wa ubora zinazofanywa.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Suleiman Murad Murad, alisema TBS lazima isimamie mipaka ya Tanzania kuhakikisha hakuna bidhaa hafifu zinazoingia na kusababisha madhara kwa watu.

"Tunataka kuwe na usimamizi na ukaguzi wa uhakika katika mipaka na bandari zote na hata kwenye njia za panya kwa sababu kuwapo kwa bidhaa zisizokuwa na viwango kwenye soko kunawafanya mwonekane hamfanyi kazi wakati mna mitambo ya kisasa," alisema Murad.

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda, alilitaka shirika hilo kutayarisha viwango vya madini kwa kuwa sasa hakuna viwango vya aina hiyo hapa nchini.

Kuhusu uhaba wa wafanyakazi wa shirika hilo, Waziri Kakunda aliahidi kuhakikisha linakuwa na wafanyakazi wa kutosha ili kusaidia kukabiliana na tatizo la bidhaa zisizokuwa na viwango nchini.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Yusuf Ngenya, shirika hilo lina wafanyakazi 470, na kwa sasa linahitaji nyongeza ya wafanyakazi 280 ili kufikisha idadi ya watumishi 750.

Waziri Kakunda alikiri kuwa shirika linahitaji wafanyakazi 750 ambao hata hivyo alisema bado ni wachache kulinganisha na majukumu ya kila siku ya shirika hilo.

Alisema kwa sasa kuna vitu vingi vinahitajika kufanywa na serikali ikiwa ni pamoja na kurasimisha bandari bubu 21 kuwa bandari halali hatua ambayo itasababisha hitaji la wafanyakazi wengine.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Ngenya, alisema shirika hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ya rasilimali watu, mishahara midogo na watumishi kutopandishwa madaraja tangu mwaka wa fedha 2016/17.

Alisema changamoto nyingine ni ufinyu wa nafasi za maabara na gharama za kununua vifaa, utayari wa umma na jumuiya ya wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa viwango katika kulinda afya na usalama wa walaji.

Dk. Ngenya alitaja changamoto nyingine kuwa ni wafanyabiashara wasio waaminifu wanaoingiza bidhaa kwa njia za panya na hivyo kusababisha uingizwaji wa bidhaa zisizo na viwango.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati hiyo, Juma Ntimizi, alishauri elimu ya viwango kwa Watanzania izidi kutiliwa mkazo ili kukabiliana na tatizo hilo.

Mjumbe mwingine wa kamati hiyo Said Kubenea, alishauri mishahara ya watumishi wa shirika hilo iboreshwe ili kuwaondolea vishawishi vya rushwa watumishi hao.

Habari Kubwa