TCRA kuibana mitandao ya kijamii

22Apr 2018
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
TCRA kuibana mitandao ya kijamii

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeviagiza vyombo vya habari nchini ikiwamo mitandao ya kijamii kuanza kujisajili kuanzia kesho.

Imesema wahusika wanapaswa kujisajili kabla ya Mei 5, mwaka huu, kwa mujibu wa kanuni ya nne ya maudhui mtandaoni ya mwaka 2018.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba, kila mwombaji atatakiwa kulipa ada ya maombi Sh. 100,000 ambayo haitarudishwa.

Taarifa hiyo ilivitaja vyombo hivyo kuwa ni vya  blogs, majukwaa mtandaoni, redio na televisheni za mtandaoni.

Alisema waombaji watakaokidhi vigezo na masharti ya usajili, watajulishwa ili walipie ada ya mwanzo ya leseni na kupewa leseni zao.

“TCRA imepewa dhamana ya kuandaa na kutunza Rajisi ya watoa huduma za maudhui kupitia blogu, majukwaa mtandaoni, redio na televisheni mtandaoni, kuchukua hatua kunapotokea ukiukaji wa kanuni tajwa na pia kuelimisha umma kuhusu kanuni hizo,” alisema.

Juzi wakati Rais John Magufuli akiwaapisha Majaji wapya 10, Wakili Mkuu wa Serikali, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka , alisema kuna ugonjwa wa ambao umeingia nchini wa watu kudhani kwamba kila kinachoandikwa kwenye mitandao ya kijamii ni cha kweli.

Alisema hayo yote yamesababishwa na uhuru wa watu kutuma vitu kwenye mitandao hiyo bila kudhibitiwa.

Rais Magufuli alisema kwa kuwa Tanzania haina uwezo wa kuidhibiti mitandao hiyo, wako watu nje ya nchi ambao wanaitumia kwa maslahi yao bila kujali madhara yanayoweza kutokea.

Habari Kubwa