TCRA kutoza faini makampuni sita ya simu

17Feb 2021
Dotto Lameck
Dar es Salaam
Nipashe
TCRA kutoza faini makampuni sita ya simu

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imezipiga faini ya shilingi bilioni 38.1 kampuni sita za simu kwa kosa la kutofikia viwango vya ubora wa huduma kama ilivyoanishwa na kanuni za ubora wa huduma za mwaka 2018.

Mkurugenzi wa TCRA, James Kilaba.

Mkurugenzi wa TCRA, James Kilaba, amezielekeza kampuni hizo kutozipeleka fedha hizo TCRA badala yake wazitumie kwa kuwekeza na kuboresha ubora wa huduma ndani ya siku 90.

Kampuni zilizopigwa faini ni pamoja na Airtel iliyotakiwa kulipa faini ya bilioni 11.5, Tigo sh bilioni 13, Halotel sh bilioni 3.4, Vodacom sh bilioni 7.8, Zantel sh bilioni 1 na TTCL sh bilioni 1.3.

“TCRA imeazimia kwamba badala ya kulipwa fedha hizo, tuzielekeze kwa watoa huduma, hivyo kila mtoa huduma atumie kiasi chake alichotakiwa kulipa, akiwekeze katika kuboresha huduma.” amesema Kilaba.

Kilaba amesema adhabu hiyo imetolewa baada ya mamlaka hiyo kupima ubora wa huduma za mawasiliano katika robo ya mwisho ya mwaka 2020 na kubaini kuwa watoa huduma hao hawakufikia baadhi ya vigezo vya viwango vya ubora.