TCRA yafafanua umiliki laini moja

03Jul 2020
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
TCRA yafafanua umiliki laini moja

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imetoa ufafanuzi wa urasimishaji umiliki laini za simu zaidi ya moja katika mtandao mmoja.

Ufafanuzi huo umetolewa baada ya kuanza rasmi utekelezaji wa kanuni za umiliki wa laini ulioanza Julai mosi, mwaka huu.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa kwenye gazeti hili na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, mtu binafsi anatakiwa kumiliki laini moja kwa ajili ya kupiga simu za sauti, kutuma ujumbe mfupi pamoja na matumizi ya data.

Vile vile, idadi ya laini zisizodhidi nne kwa kila mtoa huduma za mawasiliano kwa matumizi ya mawasiliano kati ya mashine na mashine.

Tangazo hilo lilibainisha kuwa kwa kampuni au taasisi idadi ya laini zisizozidi 30 kwa kila mtoa huduma za mawasiliano kwa ajili ya kupiga simu za sauti, kutuma ujumbe mfupi pamoja na matumizi yake.

Pia, idadi ya laini isiyozidi 50 kwa kila mtoa huduma za mawasiliano kwa matumizi ya mawasiliano kati ya mashine na mashine.

Laini zilizosajiliwa kwa matumizi yaliyoainisha kwenye kanuni, hazipaswi kutumiwa kwa kubadilishana, na kwamba wanaweza kuruhusiwa kusajili na kumiliki laini zaidi zilizoainishwa kwa kuomba na kupata idhini kutoka TRCA.

Mamlaka hiyo ilifafanua kuwa, yeyote atakayekiuka masharti ya kanuni hizo atakuwa ametenda kosa la jinai.

“Utaratibu wa kuomba idhini ya umiliki wa laini za simu zaidi ya moja katika mtandao mmoja unaendelea,” alisema.
Kadhalika Julai 31, mwaka huu, utakuwa mwisho kwa wanaomiliki laini zaidi ya moja katika mtandao mmoja.

“Utaratibu wa kuomba idhini ya kumiliki laini mpya za ziada katika mtandao mmoja unaendelea na mteja anaweza kupata huduma kupitia wakala au kwenye ofisi za watoa huduma, kwa njia za kielektroniki, mtoa huduma atawasilisha maombi ya mteja wake,” ilifafanuliwa.

Imeandikwa na Faudhia Sultan na Magdalena Haule, UDOM

Habari Kubwa