TCRA yashusha rungu vyombo vya habari

15Aug 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
TCRA yashusha rungu vyombo vya habari

KAMATI ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imevishushia rungu vyombo vya habari vya utangazaji tisa kutokana na makosa mbalimbali ya ukiukaji wa kanuni za utangazaji wa redio na televisheni na maudhui ya mitandaoni.

Watoa huduma hao walikumbwa na rungu hilo ni Carry Mastory Media Ltd, Triple A FM, CG FM; Wasafi Media Online TV; Clouds FM Radio; Radio One; Radio Free Africa; Kiss FM Radio; na Abood FM Radio.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui wa TCRA, Joseph Mapunda, alisoma uamuzi wa kamati hiyo jana jijini Dar es Salaam, mbele ya waandishi wa habari.

Mapunda alitaja adhabu zilizotolewa kwa vyombo hivyo ni kufungiwa kwa kipindi cha Jahazi cha Clouds Redio, vituo viwili vya redio kutozwa faini ya Sh. milioni tano kila kimoja, vingine kupewa onyo kali na kuwa chini ya usimamizi wa mamlaka.

Alikitaja kituo cha redio cha Clouds Entertainment kufungiwa kutangaza kipindi chake cha Jahazi kwa kosa kwa kutangaza kipindi chenye maudhui ya lugha isiyo na staha na yenye kuhamasisha ufanyaji wa vitendo vya ngono, kujichua au kupiga punyeto.

Alisema Clouds Radio walitenda kosa hilo, Juni 26, mwaka huu, la kukiuka kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Utangazaji wa Redio na Televisheni, 2018 Na. 11 (1) (c), 12(1) (a), (d) na 14 (a), (b) na (c).

Alisema Kwa mujibu wa Kifungu cha 28 (1) (b) na (d) cha Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Sura ya 172, Marejeo ya Mwaka 2017, Kamati ya Maudhui iliamua kutoa adhabu ya kukifungia kipindi cha Jahazi na kutorusha kipindi kingine chenye maudhui kama hayo kwa sababu kituo hicho kimekuwa kikionywa mara kwa mara.

Alitaja kituo kingine cha Wasafi Media Online TV, kupitia Chaneli yake ya YouTube, kilitozwa faini ya Sh. milioni tano kwa kuchapisha na kutangaza maudhui yenye lugha ya kuwakebehi wagombea mbalimbali ambao walikwenda kuchukua fomu za kugombea viti vya udiwani na ubunge na kuwafanyia Kampeni bila kuzingatia mizania, kinyume cha Kanuni Na. 7(1) (a) na (b); 12 (b).

Aidha kituo hicho pia kilitozwa faini ya Sh. milioni tano na onyo kupewa onyo kali kwa kosa la kurusha matangazo yenye maudhui yasiyo na maadili ya utangazaji kwa kuhamasisha ufanyaji mapenzi.

Mapunda alivitaja vituo vingine kuwa ni Carry Mastory Media Ltd, kilichotozwa faini ya Sh. milioni tano na onyo kali kwa kuchapisha habari za kuchochea mapenzi kinyume cha maumbile.

Alikitaja kituo kingine cha Triple A FM kilichotozwa faini ya Sh. milioni tano na kuwa chini ya uangalizi wa TCRA kwa miezi sita na kituo cha CG FM kwa kukiuka agizo la Serikali na kutozingatia mizani ya habari, wamewekwa chini ya uangalizi kwa miezi tisa.

Mapunda alivitaja vituo vingine vinne vya Radio One Stereo, Radio Free Africa, Kiss FM Radio na Abood FM Radio kwa kurusha maudhui bila kuzingatia mizania ya habari walipokuwa wakimhoji Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Tundu Lissu, kuhusu viongozi wa chama hicho kutoshiriki katika kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin Mkapa.

Mapunda alisema maudhui hayo yalirushwa kupitia vipindi vya Amka na BBC, kinachorushwa na vituo hivyo, kinyume na Kanuni Na 15(2) (b) na (c) Na. 16 za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Utangazaji wa Redio na Televisheni), 2018.

Alisema baada ya kusikiliza utetezi huo, walitoa adhabu ya onyo kwa Redio One Stereo na Redio Free Africa na kuwekwa chini ya uangalizi kwa miezi mitatu.

Alisema Kiss FM, waliwashauri kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya uandishi na utangazaji wa habari katika kazi zao na Redio Abood FM ilipewa onyo kali na kuwekwa chini ya uangalizi kwa miezi sita.

Habari Kubwa