TCRA yataja sababu luninga, redio kuomba vibali

14Aug 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
TCRA yataja sababu luninga, redio kuomba vibali

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeeleza sababu tatu za kutaka vituo vya utangazaji nchini vinavyojiunga na vituo vingine vya kanda, nje ya nchi na raia wa kigeni kuwatembelea kupata kibali kabla ya kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa kwenye gazeti hili jana, na Mkurugenzi Mkuu, lazima hiyo inatokana na mabadiliko ya kanuni ya 37, zinazoruhusu vituo vya utangazaji kujiunga na kituo chochote cha utangazaji kwa ajili ya matangazo mubashara ili mradi kunakuwa na makubaliano ya kibiashara.

Lengo ni kuweka uwazi madhumuni ya ushiriki wa raia wa kigeni katika shughuli za utangazaji wanapotembelea vituo vya utangazaji nchini.

Pia, kutimiza matakwa ya itifaki za kidiplomasia kuwa wawakilishi wa nchi za nje na mashirika ya kimataifa wanapaswa kuambatana au kupokewa kule wanapokwenda na maofisa wa serikali wanapokuwa wamepata kibali cha kutembelea miradi ambayo wanajihusisha nayo.

Kadhalika, kuhakikisha uendeshaji wa vituo vya utanagazaji unazingatia udhibiti wenye uwazi hususan kwa upande wa ufundi, ujenzi wa vituo hivyo huruhusiwa kwa kibali.

Aidha, vituo hivyo vimetakiwa kuwasilisha maombi ndani ya siku saba tangu kutolewa kwa taarifa hiyo Agosti 11, mwaka huu.

Alifafanua kuwa utaratibu huo ni wa kawaida wenye lengo la kuleta ufanisi katika usimamizi wa maudhui yanayorushwa na vituo hivyo.

TCRA ilieleza kuwa uzoefu uliopatikana katika kusimamia utekelezaji wa kanuni hiyo, kumekuwa na changamoto ya vipindi au habari zinazorushwa na vituo vya utangazaji vinapojiunga na vituo vya nje ya nchi na kurusha habari au matukio nchini.

“Kwa mfano inapotokea dhahiri kuwa habari zinazohusu nchi yetu hazikuzingatia maadili na weledi wa uandishi wa habari, huku habari hizo zikirushwa na vituo vilivyopewa leseni na TCRA, ni dhahiri inasababisha changamoto katika utekelezaji wa kanuni hizo,” alisema.

Alisema kutokana na mazingira hayo, utatuzi marekebisho ya kanuni ya 37 yamefanyika kwa kuongeza kifungu kidogo cha 2 iliyotaka kituo chochote cha utangazaji kinachojiunga na kituo kingine cha ndani au nje ya nchi kwa ajili ya kurusha matangazo yake yakiwamo ya mubashara kupata kibali/ruhusa ya kufanya hivyo kutoka TCRA.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, marekebisho hayo yanavihusu vituo vyote vya utangazaji vya redio na televisheni na watoa huduma za maudhui mtandaoni.

Habari Kubwa