TCRA yataja sababu Wanawake kuongoza kudhalilishwa mtandaoni

18Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
TCRA yataja sababu Wanawake kuongoza kudhalilishwa mtandaoni

MAMLAKA ya Mawasiliano (TCRA), imesema wanawake wanaongoza kwa kudhalilishwa mitandaoni kutokana na kuwa na tabia za kupiga picha zenye utata na kuzituma mitandaoni pamoja na kutumia simu za wapenzi wao kupiga picha za utupu.

Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi na Utekelezaji wa Sheria na Masharti ya Leseni, Dk. Philip Filikunjombe, alibainisha hayo jana wakati akizungumza katika mkutano wa wadau wa habari na wanachama wa Chama Cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC).

Alisema takwimu hizo ni kwa mujibu kesi wanazopokea katika mamlaka hiyo ambazo nyingi zinawahusu wanawake kudhalilishwa mitandaoni.

"Wanaodhalilishwa mitandaoni, dada zetu wanaongoza kwa sababu wanapenda kupiga picha na ni wachangiaji wakubwa wa masuala binafsi mitandaoni.

"Changamoto ya usumbufu wa picha zao kuchapishwa na watu wengine mitandaoni inawakuta kwa sababu ya tabia ya kutuma picha mitandaoni," alisisitiza Dk. Filikunjombe.

Aliendelea kutolea mfano kuwa waathirika wa matukio hayo wanapofika TCRA kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya waliofanya uhalifu huo, hubainika kuwa walihusika kuzichapisha wenyewe.

"Unakuta dada aliweka picha kwenye mtandao kupitia ukurasa wake na labda wakati huo alikuwa na mpenzi wake ambaye wameshaachana na pengine yeye anatakiwa azifute, lakini anakuwa hakumbuki nywila ya kuingia kwenye ukurasa wake," alisema.

Alisema suala hilo pia linachangiwa na ugawaji wa nywila kwa watu wa karibu au wapenzi wao na tabia ya kupiga picha za utupu au kuzipokea na kuzihifadhi kwenye simu.

Aliwataka Watanzania kuepuka kutuma picha za udhalilishaji mitandaoni kwa sababu ni kosa kisheria na ili kuepuka usumbufu kwa sababu teknolojia imekua na picha inavyotumwa ni rahisi watu kuichukua na kuihifadhi.

Habari Kubwa