TCU yafuta vyuo vikuu sita

22Jan 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
TCU yafuta vyuo vikuu sita

TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), imefuta vyuo vikuu sita na vituo vya vyuo vitatu kwa sababu ya kushindwa kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Charles Kihampa, akizungumza na wanahabari, jijini Dar es Salaam jana. PICHA: MIRAJI MSALA

Kati ya vyuo hivyo, viwili wamiliki wake waliomba wenyewe vifutwe ambavyo ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Yakobo (AJUCo) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Kardinali Rugambwa (CARUMUCo).

Katibu Mtendaji wa TCU, Prof. Charles Kihampa, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi ya tume ya kuvifutia usajili baadhi ya vyuo vikuu, kuendelea kusitisha udahili wa wanafunzi wapya na kurejesha udahili.

Prof. Kihampa alisema TCU imeridhia maombi ya wamiliki kufuta vyuo vikuu vishiriki viwili na vituo vitatu vya vyuo vikuu.

"Tume imeridhia maombi mengine ya kufutwa kwa vituo vishiriki vitatu kwa kusitisha utoaji wa mafunzo ambavyo ni Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji-Kituo cha Dar es Salaam (TEKU-Dar es Salaam Centre).

"Chuo Kikuu cha Mt. Yohana cha Tanzania- kituo cha Mt. Marko (SJUT- St. Mark's Centre) na Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta cha Kilimo na Teknolojia- Kituo cha Arusha (JKUAT) cha Arusha.

Alisema tume kupitia kikao chake cha cha 97 kilichofanyika juzi, imeridhia maombi yaliyofanywa na wamiliki wa vyuo na vituo hivyo kusitisha utoaji wa mafunzo.

Pia Prof. Kihampa alisema TCU imefuta hati za usajili za vyuo vikuu vitatu na Chuo Kikuu Kishiriki kimoja.

Alivitaja vyuo hivyo kuwa ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Josiah Kibira (JOKUCo), Chuo Kikuu cha Mlima Meru (MMU), Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU) na Chuo Kikuu cha Bagamoyo.

Alisema licha ya tume kutoa ushauri na mafunzo ya namna ya mbalimbali za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia pamoja na muda wa kufanya maboresho kama ilivyotakiwa.

"Kwa kuzingatia muda uliotolewa na hali ya vyuo husika ikiwa ni pamoja na changamoto ya uhaba wa rasilimali watu na fedha.
"TCU imedhihirisha kuwa vyuo hivyo havina uwezo wa kujiendesha hata vikipewa muda zaidi. Tume katika vikao vyake vya 89, 91, 92 na 97 vilivyofanyika kati ya mwezi Agosti, 2019 na Januari 2020 imefuta hati za usajili za vyuo hivyo,"alisema.

Alisema vyuo hivyo vilivyofutiwa usajili endapo wamiliki wake wataamua kujisajili wanatakiwa wasitumie majina yale yale, yanayofanana au kuelekeana kwa sababu kwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume.

Prof. Kihampa alisema mwaka 2018 TCU ilitoa muda na kuelekeza wanafunzi 2,607 waliokuwa wakisoma vyuo hivyo wahamishwe hadi mwezi Desemba 2018.

"Walifanya hivyo na vyuo hivi vilibaki bila wanafunzi kwa sababu havikuwa na ubora unaotakiwa," alisema.

Alisema tume itaendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu kuhusu hali ya ubora vyuoni.

Pia alisema kati ya mwezi Oktoba 2016 na Januari 2017 TCU ilifanya ukaguzi maalum wa kitaaluma kwa taasisi zote 64 za vyuo vikuu, vyuo vikuu vishiriki na vituo vya vyuo vikuu.

Alisema lengo lilikuwa kuhakikisha elimu ya juu itolewayo inakidhi viwango vya ubora kitaifa, kikanda na kimataifa.

Alisema matokeo ya ukaguzi yalibainisha kasoro mbalimbali katika uendeshaji wa vyuo vikuu na vyuo 45 vilikutwa na kasoro ndogo na kupewa ushauri na vilirekebisha katika kipindi kifupi na kuendelea na utoaji elimu.

"Vyuo 19 vilikutwa na kasoro kubwa, vilipewa ushauri na muda wa marekebisho ingawa havikufanya hivyo na kuzuiliwa kudahili mwaka wa masomo 2018/19.

"Hadi mwezi Oktoba 2019, vyuo vikuu vinane kati ya 19 vilivyositishwa udahili viliweza kufanya marekebisho makubwa na kuruhusiwa kudahili ambavyo ni Chuo Kikuu cha Umoja wa Afrika Tanzania (UAUT) na Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU).

Vingine ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo cha Tabora (AMUCTA), Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala Tanzania (KIUT), Chuo Kikuu Kishiriki cha Marian (MaRUCo) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Uhandisi na Teknolojia cha Mt. Yosefu (SJCET).

Alitaja vingine ni chuo Kikuu Kishiriki cha Kikristo cha Tiba Kilimanjaro (KCMUCo) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi (SMMUCo).

Prof. Kihampa alisema tume imeridhishwa na maboresho yaliyofanywa chuo Kikuu Kishiriki cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Mt. Fransisko (SFUCHAS) kilichorekebisha upungufu wa ubora na kuruhusiwa kuanzia juzi kudahili.

Pia alisema TCU imeendelea kusitisha udahili wa wanafunzi wapya kwa chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (SEKOMU) na kupewa miezi sita kukamilisha maelekezo.

"Chuo hiki kitaendelea kuwa chini ya uangalizi maalum wa tume na hakiruhusiwi kudahili wanafunzi wapya kwenye programu zote kwa ngazi zote za masomo kuanzia astashahada, stashahada, shahada, shahada ya uzamili hadi Uzamivu.

Habari Kubwa