TEC sasa kuifanya Tanzania ya kijani

08Nov 2021
Richard Makore
Mwanza
Nipashe
TEC sasa kuifanya Tanzania ya kijani

BARAZA la Maskofu Katoliki Tanzania (TEC), limezindua mpango wa miaka 13 kwa ajili ya kupanda miti katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kuifanya Tanzania kuwa ya kijani.

Uzinduzi huo ulifanyika jana jijini hapa katika mkutano uliokutanisha maaskofu wote wa Kanisa Katoliki nchini.

 Katibu wa TEC, Padri Charles Kitima, alisema, mpango huo utahusisha pia serikali na utashirikisha jamii kwa ngazi zote kuanzia familia, kitongoji na kijiji.

Padri Kitima alisema sayari ya dunia iliumbwa na Mungu na kupewa mwanadamu kuitunza na mkakati huo utalenga kutunza mazingira kwa kupanda miti.

"Mungu aliumba dunia hii na kutupatia ili tuishi sasa ni jukumu letu kuitunza kwa kupanda miti," alisema.

Alisema Tanzania ina watu milioni 60 na kila mtu akipanda miti mitatu na kuitunza itasaidia kutunza mazingira.

Aliongeza kuwa kila Parokia itatenga eneo kwa ajili ya kupanda miti pamoja na waumini wake watahimizwa kufanya hivyo.

Padri Kitima alisema watapeleka wataalamu kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wanaotaka kupanda miti na kuitunza katika maeneo yao.

Aidha, alisema mwakani Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano wa Maaskofu Katoliki 120 kutoka nchi nane za Afrika.

Alisema mkutano huo utazungumzia masuala yanayohusu mazingira ili kutoa hamasa kwa jamii bila kujali dini za watu.

Alisema maaskofu hao watatoka nchi za Sudan Kusini, Ethiopia, Zambia, Malawi, Uganda, Kenya, Eritrea na Tanzania ambao watakuwa na mkutano wa siku 10 Julai, 2022.

Awali, Rais wa TEC,Askofu Mkuu Gervas Nayisonga, akizungumza katika viwanja vya kanisani eneo la Kawekamo jijini Mwanza, alisema dhamira ya mkutano huo wa mwakani ni kuikumbusha jamii umuhimu wa kutunza mazingira.

 

Aliwaomba waumini wote wa kanisa hilo nchini kushirikiana ili kufaninikisha lengo hilo muhimu kwa nchi.

Aliwaomba wananchi kuendelea kupata elimu kuhusu utunzaji wa mazingira ili kuifanya Tanzania kuwa mahala salama kwa ajili ya kuishi leo na siku zijazo huku kukiwa na hali ya hewa nzuri.

Habari Kubwa