TEF yalaani mgambo wa Jiji kubugudhi wauzaji magazeti

23Jun 2022
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
TEF yalaani mgambo wa Jiji kubugudhi wauzaji magazeti

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limeeleza kusikitishwa na vitendo vilivyofanywa na askari wa Jiji la Dar es Salaam vya kuwanyanyasa na kuchukua meza za wauzaji magazeti wanaofanya shughuli zao maeneo mbalimbali ya jijini.

TEF imesema matukio hayo ya uonevu dhidi ya wauzaji magazeti, yamethibitishwa kufanywa na mgambo wa jiji dhidi ya wauzaji magazeti bila kuwapo sababu zilizoainishwa kufanya hivyo.

Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deodatus Balile jana, ilibainisha kuwa, Oktoba mwaka jana serikali ilianza kuwaondoa wafanyabiashara wadogo pembezoni mwa barabara za jiji hilo, lakini wauzaji magazeti hawakuondolewa kutokana na sababu za msingi.

"Siyo kwamba hawakuondolewa kwa bahati mbaya, bali waliachwa kwa mujibu wa Sheria ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya Mwaka 2014, nyongeza ya 9(3) inayotambua magazeti kuwa ni nyenzo ya elimu siyo biashara,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema sheria hiyo inafanana na sheria karibu zote za kodi ya mapato na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) duniani kote, na ndiyo maana katika miji yote kuna meza za magazeti na vitabu katika kona za mitaa kwa ajili ya kuendeleza elimu na maarifa kwa watu wake.

“Tanzania itakuwa nchi pekee duniani kuzuia watu wake wasisome magazeti na vitabu kwa kuingiza uuzaji huu wa nyenzo za elimu katika orodha ya biashara kama kitendo kilichofanywa na mgambo wa Jiji la Dar es Salaam,” alisema.

Balile alisema mbali na kueleza masikitiko hayo, TEF linamtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji hilo na wengine wenye nia kama hiyo ya kubughudhi wauza magazeti, kusitisha mara moja mpango wa kuondoa meza za wauza magazeti na kuwarejeshea meza zao walioporwa.

Alisema pamoja na kuwarejeshea meza zao pia Jiji linapaswa kuwaomba radhi Watanzania kwa uamuzi huo wa kuwakosesha nyenzo muhimu ya kujielimisha iliyoruhusiwa kwa mujibu wa sheria.

“Kuruhusu uamuzi huu kuendelea ni sawa na kuamua kwa makusudi kujenga taifa lenye kizazi cha watu wajinga, kwani maarifa yanapatikana kwa kusoma magazeti na vitabu, tunamwomba Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, kuchukua hatua za haraka kusitisha kadhia hii inayovunja sheria za nchi,” Balile alisema.

Mwenyekiti huyo alisema wahariri wanalaani kitendo hicho na kusisitiza kamwe kisirudiwe tena kwa kuwa kwa mwelekeo huo, mgambo wanataka kulisukuma taifa katika kujaribu ujinga ambao una gharama kubwa kwa sasa na baadaye.

Habari Kubwa