TEMDO yagawa vifaa vya mamilioni

13Sep 2020
Renatha Msungu
Arusha
Nipashe
TEMDO yagawa vifaa vya mamilioni

TAASISI ya Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO), imefanikiwa kusambaza viteketeza taka 20 vyenye thamani ya Sh. milioni 900 katika mikoa mbalimbali nchini.

Profesa Frederick Kahimba

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Profesa Frederick Kahimba, aliwaambia waandishi wa habari jijini Arusha jana kuwa, viteketeza taka wanavyotengeneza vinasaidia kuchuja kemikali za taka kabla moshi haujatoka kusambaa na kuharibu mazingira.

Profesa Kahimba alisema moshi unaotoka kwenye vifaa hivyo ni wa kawaida ambao hauna madhara kwa jamii.

Alitaja mikoa ambayo tayari wamepeleka vifaa hivyo kuwa ni Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Shinyanga, wakitarajia kusambaza pia katika mikoa mingine yote ya nchi.

Alisema matarajio yao ni kuona kila hospitali nchini inakuwa na kiteketeza taka za hospitali ili kuepusha uchafuzi wa mazingira.

"Tumejipanga kuhakikisha hivi viteketeza taka vinaenea kila mahali, tunahitaji kuona mazingira yanalindwa ndiyo maana tukabuni hivi viteketeza taka," alisema Profesa Kahimba.

Mjasiriamali Elizabeth Mkumbo alisema TEMDO inawanufaisha kwa kiwango kikubwa kutokana na kuwatengenezea mashine na miundombinu ya kuendeleza biashara zao.

Alisema awali walikuwa wakifanya biashara kwa shida kutokana na kukosa vifaa vya kufanyia kazi, lakini kwa sasa wanafanya kazi bila wasiwasi wowote.

"Tunaomba TEMDO waendelee kutupa sapoti katika kutusaidia, hapa tulipofikia ni kutokana na msaada wa TEMDO," mjasiriamali huyo alisifu.

Alisema wameunda kikundi ambacho wanatengeneza bidhaa kupitia mashine walizopewa na TEMDO na kwamba taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele kuwatafutia masoko.

Mhandisi Honest Lustful alisema TEMDO wanatengeneza mashine mbalimbali kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa, zikiwamo mashine za kukamulia mafuta, juisi na za kukatia mabati.

Habari Kubwa