TFDA yawa ya kwanza Afrika kukidhi vigezo vya WHO

19Dec 2018
Devota Mwachang'a
Dar es Salaam
Nipashe
TFDA yawa ya kwanza Afrika kukidhi vigezo vya WHO

MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA), imekuwa ya kwanza Barani Afrika kukidhi vigezo vya Shirika la Afya Duniani (WHO), kutangazwa kuwa taasisi iliyofikia hatua ya tatu ya ubora wa mifumo ya udhibiti wa dawa ijulikanayo kama ‘Maturity Level Three’.

Katika mkutano wa waandishi wa habari na wafanyakazi wa Mamlaka uliolenga kutoa taarifa kuhusu TFDA kufikia ngazi ya tatu ya ubora wa mifumo ya udhibiti wa dawa, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema mafanikio hayo yanatuma ujumbe kwa jamii kuwa dawa zinazothibitishwa na mamlaka zina ubora, ufanisi na usalama kwa matumizi ya binadamu.

"Kufikiwa kwa hatua hii kuna maanisha kwamba nchi yetu itaendelea kupata dawa zilizo bora, salama na fanisi...na kwamba dawa duni na bandia hazitapata nafasi ya kuwapo kwenye soko," alieleza Mwalimu.

Aliitaka Mamlaka kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kufikia ngazi ya nne kwa kuwa tayari ni taasisi iliyofikia viwango vya kimataifa (ISO 9001 na ISO/IEC 17025) kwa maabara yake.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Adam Fimbo, alieleza hatua iliyofikiwa kuwa ni kubwa kwa mujibu wa vigezo vya WHO, na kuifanya Mamlaka kuingia kwenye kundi la nchi chache duniani zilizofanikiwa kufikia hatua hiyo. Iwapo Mamlaka ikifikia hatua ya ngazi ya nne, itawezesha Maabara ya TFDA iliyoko Mwanza ipate ithibati ya ISO/IEC 17025.

"Jitihada zetu zimeendelea kuzaa matunda na ndiyo leo tunashuhudia waraka uliotolewa na WHO baada ya kuridhika kuwa mifumo yetu sasa imefikia hatua hii; haya ni matunda ya uzoefu tulioupata kupitia tathmini zilizotupatia Ithibati za ISO," alifafanua.

Aidha, Fimbo alisema tangu mwaka 2003, Mamlaka imekuwa ikiweka mikakati ya kuboresha mifumo yake ya utendaji ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mwakilishi Mkazi wa WHO, Dk. Tigest Mengestu, alisema jamii na serikali zinapoteza pesa nyingi katika kununua dawa ili kuokoa maisha ya watu, kutunza afya, kuzuia magonjwa na yale ya mlipuko; kufanikisha hayo kunahitaji usalama, ufanisi, ubora na matumizi sahihi ya dawa.

"Wadhibiti wa dawa kama TFDA wana jukumu kubwa katika kujali na kulinda afya ya jamii dhidi ya matumizi ya dawa zisizo salama...hatua iliyofikiwa na Mamlaka inadhihirisha kuwa imeboresha mifumo yake ya kuhakisha dawa zilizopo sokoni ni bora na salama," alisema Mengestu.

Mamlaka imetambulika kufikia viwango vya ngazi ya tatu baada ya wataalamu kutoka WHO kufika TFDA mwezi Novemba, mwaka huu kufanya tathmini ya mwisho.

Habari Kubwa