TFS yahimiza utunzaji misitu

19Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
TFS yahimiza utunzaji misitu

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) umewahimiza Watanzania kuendelea kutunza misitu kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho na kusisitiza changamoto zilizopo zitatuliwe kwa majadiliano na hatimaye misitu ibaki salama.

Meneja wa Rasilimali za Misitu, Dk. Masota Abel, alisema hayo juzi kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo, baada ya kumalizika kwa kikao cha majadiliano  kati ya maofisa wa TFS na ujumbe wa watu 15 kutoka Ethiopia ambao walikuja kujifunza namna nzuri ya utunzaji misitu.

Waethiopia hao wametoka katika taasisi mbalimbali zinazohusika na utunzaji misitu na utafiti katika nchi yao na walipata fursa ya kwenda katika maeneo mbalimbali katika mikoa ya Tanga, Morogoro, Iringa na Dar es Salaam.

 Dk. Abel alisema ni vyema Watanzania wakahakikisha wanatunza misitu iliyopo na kufafanua wageni hao kutoka Ethiopia wamefurahishwa na TFS inavyotunza misitu, hivyo kuwaomba Watanzania kuwa sehemu ya kila mmoja kwa nafasi yake kuitunza kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.

"Ujumbe wangu kwa Watanzania watunze misitu. Tuitunze kwa kufuata taratibu zinazostahili na hata kama kuna changamoto zingine tutumie nafasi za majadiliano kutafuta ufumbuzi na hatimaye ibaki salama. Tuache kuvamia misitu na kuikata, tuache kufanya shughuli za kilimo maeneo ya hifadhi na misitu kwa ujumla.

"Tunapaswa kufahamu misitu tuliyo nayo nchini ni keki ya taifa, hivyo lazima tuitunze na ilete tija kwa ajili ya kizazi kilichopo sasa na kijacho. Kwetu TFS tutaendelea kuweka mikakati ya kuhakiksha misitu inabaki salama, lakini wakati huo huo wananchi nao wanalo jukumu kama hilo," alisema.

Kuhusu changamoto kubwa ambayo TFS inakabiliana nayo, Dk. Abel alisema ni ongezeko la watu ambalo linasababisha ukosefu wa nishati mbadala ya miti ambayo itakidhi mahitaji, jambo ambalo limesababisha misitu kuvamiwa na kuharibiwa.

Pia alisema ongezeko la watu limesababisha kuwe na mahitaji makubwa ya ardhi, hivyo wengi kuvamia maeneo ya misitu yaliyohifadhiwa. Pia alisema mabadiliko ya tabianchi nayo yanachoche watu kuvamia misitu kwa lengo la kutafuta ardhi yenye rutuba kwa shughuli za kilimo.

Kuhusu kwa nini Waethiopia hao wameichagua Tanzania, Dk. Abel alisema nchi hii inasifika kwa utunzaji wa mazingira, hivyo wameona ni sehemu sahihi ya kujifunza kuhusu uhifadhi wa misitu.

"Wageni wetu wamekiri na kukubali kazi nzuri ambayo inafanywa na serikali yetu kupitia TFS katika kutunza misitu. Wameeleza namna kile ambacho wamejifunza watakavyokwenda kwao kuweka mikakati itakayowawezesha kuitunza misitu yao. Ethiopa misitu yao imeendelea kuharibiwa.

Tunaweza kusema hawana misitu tena. Kwao eneo kubwa limebaki kuwa jangwa ndiyo maana wanasema hata asali yao wanafuga katika mabanda na hiyo inasababisha asali kutoka Tanzania inabaki kuwa bora na ya asili kuliko ya kwao," alisema.