TGNP kuandaa elimu juu ya vifurushi vipya vya Bima ya afya

09Dec 2019
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
TGNP kuandaa elimu juu ya vifurushi vipya vya Bima ya afya

MTANDAO WA Jinsia Tanzania (TGNP), umesema unandaa elimu kwa jamii kuhusu masuala yanayohusu huduma za afya hususani vifurushi vipya vilivyozinduliwa hivi karibuni na Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF).

mkurugenzi mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi, picha mtandao

Akizungumza mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, kwenye semina za jinsia na maendeleo (GDSS), mkurugenzi mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi, alisema kumekuwa na maswali mengi kuhusu huduma za afya.

Alisema wananchi bado hawajajiunga na huduma zinazotolewa na mfuko huo, kwa kutofahamu umuhimu au gharama zilizowekwa.

Hivi karibuni NHIF, ilizindua vifurushi tofauti ikiwamo Najali Afya kinachoanzia 192,000 kuanzia umri wa miaka 18 hadi 35, Timiza Afya (384,000) na Wekeza Afya (516,000) vinavyotoa huduma kulingana na idadi na umri pamoja na wategemezi.

“Wanaharakati mliopo leo katika semina hii ni wangapi mnatumia huduma hizi, afya ndio kila kitu, afya ikiwa nzuri ni rahisi kufanya maendeleo, tutawaleta wataalamu ili watoe elimu kuhusu afya hapa GDSS,” alisema Liundi.

Awali akiwasilisha mada kuhusu ukatili wa kijinsia, Anna Kikwa kwenye semina hiyo iliyobeba ujumbe wa ‘Nafasi ya jamii katika vita ya kutokomeza ukatili wa kijinsia, alisema elimu inahitajika kwa kushirikana na wadau wengine ili kuleta nguvu ya pamoja.

“Ili tufanikiwe katika kupinga ukatili wa kijinsia tunapaswa kufanya kwa pamoja, jamii na wadau ili kutokomeza matukio ya ukatili,” alisema Kikwa.

Naye Mwanaharakati Janeth Mawinza alisema kuanzishwa kwa madawati ya kijinsia kuanzia ngazi ya mitaa itasaidia taarifa kutolewa bila vikwazo.

Alisema baadhi ya wanakumbwa na ukatili huo wanapatwa na woga wa kufika polisi na kwamba unazishwaji wa madawti mtaani kutaongeza takwimu za taarifa zinazotokea kwenye jamii.

“Kuwepo na motisha wa wanaharakati ambao wamekuwa wakipambana na hata kuhatarisha maisha yao , binafsi nilifikia kuhatarisha maisha wakati nikifuatilia kesi fulani kuhusu ukatili wa kijinsia," alisema Mawinza.

Habari Kubwa