THRDC yaainisha mambo 10 hatari kwa uhai wa Azaki

24Jun 2019
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
THRDC yaainisha mambo 10 hatari kwa uhai wa Azaki

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umeainisha mambo 10 hatarishi kwa uhai wa Azaki katika muswada wa marekebisho ya sheria zinazosimamia mashirika ya kiraia nchini (NGO).

Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa.

Aidha, umeshangazwa na dharura ya serikali kupeleka rasimu ya marekebisho iliyotengenezwa kwa siku 50, lakini siku mbili kabla ya kupelekwa bungeni yaliwekwa kwa Azaki na kunyimwa haki ya kushiriki mchakato mzima wa utengenezaji.

Kwa mujibu wa uchambuzi huo uliotolewa na Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, hakuna anayejua dharura ya serikali imebeba dhamira gani kwa Azaki.

Alisema muswada unafuta tafsiri ya mashirika yasiyo ya kiserikali na kuweka ufafanuzi mpya ambao hautambui nyanja ya ulinzi na uendelezaji wa haki za binadamu.

Pia, haujumuishi kampuni zenye dhamana, makundi madogo ya uwekezaji (Vikoba kwa ujumla), mashirika ya dini, na kwamba hayawezi kuwa kampuni zisizofanya biashara na kwamba ni lazima wafanye biashara au uwekezaji ili usajiliwe kama kampuni yenye dhamana.

Pili: Kuondolewa usajili moja kwa moja; kwamba muswada umeongeza kifungu kinachofuta usajili wa NGO zilizosajiliwa chini ya sheria hiyo, ambayo hayajajumuishwa kwenye ufafanuzi mpya ndani ya miezi miwili baada ya muswada kupitishwa kuwa sheria.

Uchambuzi huo ulisema muswada huo maalum wa sheria zilizoandaliwa, marekebisho mchanganyiko ulipelekwa chini ya hati ya dharura bungeni Juni 19, mwaka huu na kuwanyima haki ya kushiriki mchakato wa utengenezaji wa muswada huo.

"Hatua hii inakiuka uhuru wa kujumuika, njia mbadala zitolewe kwa mashirika haya halali kuhamia katika upande unaowafaa na siyo kufutiwa usajili moja kwa moja," alisema Olengurumwa.

Tatu: NGO kusimamishwa kabla ya kusikilizwa; muswada huo umeongeza vipengele vinavyohusu kusimamishwa NGO wakati wanaongejea suluhu ya bodi, kitu ambacho ni kinyume na kanuni za haki, dhana ya kutokuwa na hatia mpaka ithibitishwe.

Nne: Mamlaka ya Msajili kufuatilia na kutathmini mashirika yasiyo ya kiserikali kila robo mwaka; kwamba imeongezwa kipengele kinachompa msajili mamlaka makubwa ikiwamo kufuatilia na kutathimini NGO kila baada ya robo mwaka .

"Mamlaka kama haya yanaweza kutumika kiholela na kwa kuonea, ni vigumu kutembelea mashirika yote nchini," alisema Mratibu huyo.

Tano: Mamlaka ya Msajili kufanya uchunguzi; kwamba muswada umempa uwezo msajili kuchunguza NGO kwa kushirikiana na vyombo vya dola, na kwamba yanahusishwa na udhibiti unaoangalia haki ya faragha na uhuru.

"Msajili wa NGO hapaswi kupewa mamlaka chini ya sheria nyingine kufanya uchunguzi wa uhalifu, wigo wa sheria yoyote iliyoandikwa haujulikani na hii inaweza kuvutia matumizi mabaya ya mamlaka na kusababisha kukamatwa kiholela na kuingiliwa," ilifafanua.

Sita: Kuondolewa kwa usajili wa kudumu, marekebisho hayo yanapendekeza NGO kujisajili tena baada ya miaka kumi, kupata upya hati zao baada ya miaka 10 na kwamba ni mzigo kiuchumi na kiutawala na ofisi ya msajili.

Aidha, Olengurumwa alisema utaratibu huo unaondoa uhuru wa mashirika yasiyo ya kiserikali na kujenga woga na udhibiti binafsi.

Saba: Mamlaka ya kutamka kuwa asasi ni hatari, marekebisho hayo yanampa mamlaka waziri kutamka kuwa asasi ni hatari kwa utawala bora nchini, na kwamba halitakuwa halali, kipengele ambacho kinaziacha NGO katika hatari ya matumizi mabaya ya mamlaka.

Nane: Kuzilazimisha NGO kuwa kibiashara, kwamba zitasajiliwa chini ya sheria za kampuni zenye dhamana ambazo hazikuomba hati ya ukubalifu yanatakiwa kukubaliana na Sheria ya Kampuni na kuwa mashirika ya kibiashara vinginevyo yatafutwa.

Tisa: NGO na Azaki yenye hati ya ukubalifu kusitishwa ndani ya miezi miwili; kwamba kampuni yenye dhamana iliyosajiliwa chini ya sheria ya kampuni yenye hati ya ukubalifu na chini ya Sheria ya NGO itachukuliwa kuwa imesajiliwa chini ya Sheria ya NGO na kuondolewa katika orodha ya kampuni ya Msajili wa kampuni.

Kumi: Asasi kuondolewa usajili ndani ya miezi mwili; kwamba asasi yoyote iliyosajiliwa chini ya sheria ya asasi ambayo haiendani na ufafanuzi au tafsiri iliyotolewa kwenye muswada litafutwa.

"Shirika lisilo la kifuasi, lisilo la kibiashara litaondolewa usajili moja kwa moja ndani ya miezi miwili baada ya muswada wa sheria kupita," alisema Olengurumwa.

Habari Kubwa