THRDC yawatambua wanawake 10 vinara haki za binadamu

08Mar 2018
Onesmo Olengurumwa
Nipashe
THRDC yawatambua wanawake 10 vinara haki za binadamu

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) katika kuazimisha siku ya wanawake duniani imetoa orodha ya baadhi ya wanawake 10 ambao wamekuwa vinara wa kupigania haki za binadamu kwa mwaka 2017/2018.

Onesmo Olengurumwa.

Siku ya wanawake duniani huazimishwa kidunia tarehe 8 kila ya mwezi Machi kila mwaka. 

Siku wanawake duniani ni siku ambayo wanawake wanatambuliwa kwa mafanikio yao bila kujali tofauti zao za kitaifa, kikabila, lugha, tamaduni, hali za kiuchumi, au kisiasa. 

Hivyo, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania unaungana na wanawake wote duniani katika kusherehekea siku hii ya adhimu ya Wanawake Duniani. 

Kauli mbiu ya mwaka huu ni *“Sukuma* *Maendeleo”.* Kwa sababu ya kauli mbiu hii, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania unapenda kupazia sauti juu ya jitihada za wanawake watetezi wa haki za binadamu Tanzania pamoja na jitihada zingine ambazo zimechukukuliwa kuhakikisha wananwake watetezi wa haki za binadamu Tanzania wanaendelea kufanya kazi zao bila vitisho au hofu yoyote.

Baadhi ya ya matukio ya ukiukwaji wa haki za wanawake yanahusisha; ukatili wa kijinsia, haki ya urithi, haki ya kuwa na maamuzi na kuhusishwa kwenye uongozi, haki ya kumiliki mali/ardhi, haki ya kuwa na elimu bora na fursa mbali mbali za maendeleo.

 

1/ Mama Samia Suluhu Hassan

Mama Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mpiganaji wa haki za wanawake na watoto Tanzania.

2/ Halima Mdee 

Halima Mdee, Mbunge wa Kawe, mwanamke mahiri na mwanasiasa anayepigania haki za kisiasa kwa wanawake.

3/Daktari Hellen Kijo Bisimba 

Daktari Hellen Kijo Bisimba, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ambaye ni mpigania haki za binadamu mkongwe na amekuwa mstari wa mbele katika kupigania Utawala wa sheria, Demokrasia na uchaguzi huru na wa haki.

4/ Wakili Fatma Katume

Wakili Fatma Katume, Wakili wa Kampuni wa Mawakili ya IMMMA; mtetezi wa haki za binadamu ambaye amekuwa akitumia taaluma yake ya sheria katika kuhakikisha heshima juu ya haki, utawala wa sheria, demokrasia, na uchaguzi huru na waki.

5/Vicky Ntetema

Vicky Ntetema, Mkurugenzi Mtendaji wa Under the same Sun, shirika la kutetea haki za watu wenye ualbino ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watu wenye ualbino Tanzania wanaishi katika mazingira salama.

6/ Rose Sarwatt

Rose Sarwatt, Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Wanawake Wajane Tanzania (TAWIA) ambaye binafsi na kwa kutumia miradi inayofadhiliwa na wafadhili amekuwa kinara wa kutetea haki za wanawake wajane Tanzania.

7/ Maria Sarungi Tsehai

Maria Sarungi Tsehai, Mkurugenzi Mtendaji wa Change Tanzania; mtetezi wa haki za wanawake ambaye amekuwa wakala wa mabadiliko na kuhakikisha sauti za wasiosikika zinasikika kupitia mitandao ya kijamii.

8/Salma Said

Salma Said, Mwandishi wa Habari- Mtetezi wa haki za wanawake ambaye amekuwa akitumia mitandao ya kijamii na uandishi wa habari kuibua ukiukwaji wa haki za kisiasa na kijamii Zanzibar.

9/ Jane Magigita

Jane Magigita, Mkurugenzi Mtendaji wa Equality for Growth; Mtetezi wa haki za Wanawake na mpigania maendeleo na uhusishwaji wa wananchi katika mambo yanayowahusu.

10/ Maanda Ngoitiko

Maanda Ngoitiko, Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la wanawake wafugaji (PWC) vijijini ambaye pamoja na vitisho mbali mbali vya kila siku, ameendelea kutetea haki ya ardhi kwa watu wa vijijini wilaya ya Ngorongoro.

Wakati tunawatambua na kuwapongeza wanawake wakongwe wanaopigania haki za binadamu Tanzania katika nyanja mbali mbali, Mtandao unapenda pia kuwainua wanawake chipukizi wapigania haki za binadamu kama vile,

1/Faraja Nyalandu.

2/ Elsie Eyakuze.

3/ Rebecca Gyumi.

4/ Angela Benedicto.

5/ Carol Ndosi.

6/ Ummy Nderinago.

 

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania unapenda kuwaasa wanawake watetezi wa haki za binadamu Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya yafuatayo;

·         Kupaza sauti juu ya kauli mbiu ya mwaka huu juu ya “Sukuma Maendeleo”

·         Kutetea haki za wanawake kwa kuwahamasisha watungaji wa sheria kuhakikisha wanatunga sheria zinazowatambua wanawake kama chachu ya maendeleo, kuzithamini kazi za mwanamke, na kuhakikisha ulinzi wa wanawake watetezi wa haki za binadamu dhidi ya madhila mbali mbali wanayopitia katika utekelezaji wa shuhuli zao. Hii itasaidia kuhakikisha ulinzi wa haki za wanawake na haki zingine kwa ujumla.

·         Kupigania madabiliko ya sheria kandamizi na zenye ubaguzi ambazo zinaathiri wanawake watetezi wa haki za binadamu.

·         Kuendelea kupinga ubaguzi wa kijamii, kiutamaduni, kidini, na kiuchumi ambao unapelekea wanawake kuwa katika hatari mbali mbali wakati wanatekeleza majukumu yao.

·         Kufanya kazi kwa umoja na kuwa na sauti moja katika kupigania haki za wanawake. Wanawake wakiwa na sauti moja itakuwa rahisi kuongeza nafasi ya wanawake Tanzania na kwa namna hiyo chochote wanachopigania wanawake kitaweza kusikika na kutekelezwa haraka.

·         Kudumisha ushirikishwaji wa wanawake kama wadau muhimu sawa na wanaume ili kuhakikisha maendeleo endelevu, amani, usalama na kuheshimu haki za binadamu.

·         Kuwawezesha wanawake kama nguzo muhimu juu ya changamoto za kuhakikisha ustawi wa kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni Tanzania.

 

Imetolewa leo tarehe 8/03/2018

Na: Onesmo Olengurumwa

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)

 

Habari Kubwa