TIB yatuliza wateja wake

16Jul 2019
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
TIB yatuliza wateja wake

BENKI ya TIB Corporate imewatoa wasiwasi wateja wake nchini kuwa haiko chini ya usimamizi wa benki bali mabadiliko ya uongozi wa juu yaliyofanywa ni ya kawaida.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Fred Luvanda.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Fred Luvanda, wataendelea kutoa huduma kama kawaida kwa ubora na ufanisi wa hali ya juu.

Kabla ya uteuzi huo Luvanda alikuwa Msimamizi wa Sekta ya Fedha, na taarifa iliyotolewa juzi na BoT,  ilieleza kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Frank Nyabungege, amesimamishwa kwa kile kilichoelezwa ni mwenendo usioridhisha wa benki hiyo.

“Tunawatoa wasiwasi wateja na wadao wote wa benki ya Biashara TIB na wananchi kwa ujumla, wajue kuwa huduma zinaendelea kama kawaida,” alieleza na kuongeza:

“Pia mfahamu kuwa serikali na Benki Kuu inatambua umuhimu wa benki hii, itaendelea kitoa ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha benki inazidi kuboresha huduma zake na kukua kwa maendeleo ya nchi yetu.”

Aidha, aliitaka menejimenti na wafanyakazi kuendelea kufanyakazi kwa bidii ili kuhakikisha benki inatimiza malengo yake.

TIB Corporate inamilikiwa na serikali, na inatoa huduma zote za kibenki za kibiashara kwa mashirika na taasisi za aina mbalimbali za serikali na binafsi.

Benki hiyo ina matawi saba kwa sasa ya  Dar es Salaam matatu, Mwanza, Arusha, Mbeya na Dodoma.