Tibaijuka atangaza kung’atuka ubunge

06Jul 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Tibaijuka atangaza kung’atuka ubunge

MBUNGE wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka, ametangaza kujiweka kando katika masuala ya siasa huku akisema hatagombea tena ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

MBUNGE wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka.

Katika mahojiano maalum na ‘blog’ ya Millard Ayo, Prof. Tibaijuka alisema anastaafu kwa sababu yeye ni kizazi cha Mwalimu Julius Nyerere ambaye aliwafundisha kung’atuka.“Mimi 2020 ninastaafu, ninang’atuka kwa sababu sisi ni kizazi cha Mwalimu Nyerere na katika vitu alivyotufundisha ni kung’atuka,” alieleza Prof. Tibaijuka katika mahojiano yake hayo.

Alipouliza kama sababu ni kuhofia kushindwa katika uchaguzi ujao, alisema hakuna anyemhofia kwa sababu mwaka 2015 alipita katika uchaguzi licha ya kuwapo kwa ushindani mkubwa.

“Katika uchaguzi wa 2015, Muleba Kusini pamoja na kampeni ya Escrow bado nilipita kidedea. Kwa kweli nawashukuru wananchi wa Muleba. Ni watu wanaotafuta maendeleo, wana kiu ya maendeleo,” alisema Prof. Tibaijuka na kuongeza kuwa:“Ninaposema nastaafu ubunge haimaanishi kwamba nastaafu Muleba, hivi ni vitu viwili tofauti. Mimi  ninastaafu uwakilishi, Bunge letu hili lingekuwa Seneti ningesema nitaendelea,” alisema Prof. Tibaijuka

Alisema kwa sabababu Bunge linalinda maslahi mapana ya umma hawezi kuwania tena ingawa anaamini atapatikana mwakilishi mzuri kutoka jimbo hilo.Alisema mwaka 2015 kulikuwa na kampeni chafu dhidi yake lakini wananchi wa Muleba waliamuamini katika kipindi chote cha miaka 10 hivyo anaamua kung’atuka kwa utashi wake.

“Mimi kama kupigwa chini ningepigwa chini mwaka 2015. Asiyekubali kushindwa si mshindani, kwa hiyo mimi sistaafu kwa ajili ya hofu, kwanza Muleba anayenishinda ni nani? Ni Mwenyezi Mungu peke yake.

“Kwa kipindi cha miaka 10 nimejifunza, nimeelewa matatizo ya wananchi na wakati ule nilipotoka Umoja wa Mataifa, nilikuja na nia moja ya kujifunza kwamba taifa letu lina tatizo gani na tufanye nini ili tuweze kusogea mbele,” alisema.

“Kwa hiyo hata bungeni ninaposimama, nikiona kitu hakijakaa sawa huwa sisimami kiitikadi. Pia sitaki ushabiki ambao hauna mantiki,” alisema Prof. Tibaijuka.

Mwanasiasa huyo na mchumi nguli, aliwaasa wagombea ambao watataka kuwania nafasi hiyo katika jimbo hilo kuwa wastaarabu na kuacha pupa kwa sababu wananchi wake ni waelewa. 

“Wanaotaka kugombea waje kwa adabu wasije kwa jazba, fitina na mbinde,” alisema Prof. Tibaijuka.

Prof. Tibaijuka pia aliahidi kujikita katika kusaidia wanawake na wasichana ambao hawafahamu haki zao kwa ajili ya kuepuka matukio ya ukatili wa kijinsia na mauaji ya vikongwe.

Alisema pia katika umri wake wa kustaafu ubunge akiwa jimboni kwake, atajikita kutoa elimu ya kujitambua kwa wasichana na wanawake ambao hawazifahamu haki zao katika jimbo hilo.

Habari Kubwa