TIC yajipanga kuibua fursa kupitia SGR

18Sep 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
TIC yajipanga kuibua fursa kupitia SGR

MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dk. Maduhu Kazi, amekutana na wadau kuangalia namna ya kuibua fursa za kiuchumi pembezoni mwa mradi wa reli ya kisasa (SGR) pindi itakapoanza.

Wadau hao ni pamoja na Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Akizungumza kwenye kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma juzi, Dk. Kazi alisema wamekutana, ili kuandaa mpango wa kuibua fursa za uwekezaji zinazotokana na kuwapo kwa mradi huo.

Dk. Kazi alisema TIC imeona ni vyema kuibua fursa au shughuli za kiuchumi zinazotakiwa kufanyika katika maeneo ya pembezoni mwa reli.

Alisema hiyo itasaidia kuleta ufanisi na tija kwa reli na jamii iliyopo pembezoni.

“Uwapo wa reli hii ni mojawapo ya maboresho ya mazingira ya uwekezaji kwenye miundombinu yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli,” alisema.

Dk. Kazi alisema kwa mujibu wa Sheria ya Uwekezaji Na. 26 ya mwaka 1997, miongoni mwa majukumu ya TIC ni kuibua, kuhamasisha na kunadi fursa za uwekekezaji nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, alisema wako tayari kutoa ushirikiano, ili kufanikisha malengo ya kuhakikisha reli hiyo inaleta manufaa zaidi kwa jamii iliyopo pembezoni mwa reli.

Naye Kamishna Mkuu wa TRA, Dk. Edwin Mhede, alisema mpango huo unapaswa kushirikisha sekta binafsi na wadau wengi wa sekta binafsi na serikali.

“Mpango huu ni mzuri wenye nia ya kuifanya reli yetu isiishie kubeba mizigo na abiria tu bali iende sambamba na faida zingine za kiuchumi, uwekezaji pamoja na elimu kwa mlipakodi, ili kukusanya mapato ya serikali bila kuwaletea usumbufu wawekezaji,” alisema.

Habari Kubwa