TIC yajivunia miaka 3 ya JPM

06Dec 2018
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
TIC yajivunia miaka 3 ya JPM

KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kwa miaka mitatu kimesajili miradi 905 ya wawekezaji wazawa na wa kutoka nje yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 13.2.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geoffrey Mwambe, akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, kuhusu mafanikio makubwa katika sekta ya uwekezaji katika miaka mitatu ya serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli. PICHA: JOHN BADI

Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Geofrey Mwambe, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizungumzia mafanikio ya TIC ya miaka mitatu tangu Rais John Magufuli aingie madarakani.

Alisema miradi hiyo ambayo ipo ya miaka mitatu hadi mitano, itakapokamilika itatoa ajira za moja kwa moja kwa Watanzania 115,055.

“Mafanikio haya yametokana na Rais Magufuli tangu aingie madarakani amepambana na vitendo vya rushwa, ameondoa urasimu uliokuwapo ndani ya taasisi za serikali, ametekeleza ujengwaji wa miundombinu, ujenzi wa viwanda kupitia mpango wa maendeleo wa miaka mitano. Mapambano haya yameturahisishia TIC kuvutia uwekezaji ndani na nje ya nchi kwa urahisi,” alisema.

Alisema TIC kwa kipindi cha miaka mitatu, imeongeza kasi ya uwekezaji na kuitangaza nchi kimataifa kwa sababu taswira yake kwa wawekezaji wa nje imebadilika na kuona ni eneo sahihi la kuwekeza.

“Watanzania wanatakiwa kutambua kuwa tunapambana na mataifa makubwa ambayo kila moja linavutia uwekezaji eneo lake,” alisema.

Alisema tangu Novemba mwaka 2015 hadi Oktoba mwaka huu, TIC imesajili miradi 905 ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Alisema miradi ya wawekezaji wa ndani iliyosajiliwa ni 307 ambayo imekidhi vigezo vilivyowekwa kwa sheria ya sasa ya kuwa na mtaji usiopungua dola 100,000 (Sh. milioni 230).

Alisema miradi ya wawekezaji wa nje iliyosajiliwa ni 319, ambapo inamtaka mwekezaji awe na mtaji wa Dola za Marekani 500,000.
Alisema ipo miradi ambayo mwekezaji wa nje anaweza kuwa na mtaji chini ya dola 500,000 ambao sheria iliyopo hawatakiwi kwenda TIC kusajiliwa.

“Changamoto hii tumeiona tupo kwenye mchakato wa kurekebisha sheria, jambo hili lipo mikononi kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, tunaamini itarekebishwa kwa kasi ili TIC  wawekezaji wote wasajiliwe TIC.

Alitolea mfano siku moja alikwenda wilaya moja na kukuta mzawa amewekeza shule nzuri ya kimataifa ya kisasa, lakini hana habari na TIC wala hajajisajili licha ya kuwa na mradi mkubwa.

Alisema baada ya marekebisho ya sheria TIC itashughulika na miradi yote ya uwekezaji ikiwamo miradi ya madini, mafuta, gesi na kemikali hatarishi ambayo awali, kituo hicho kilitakiwa kisiiguse.
 
Pia mkurugenzi huyo alitaja miradi mingine ya ubia 277 ambayo wawekezaji wa nje wameomba kushirikiana na wazawa.

Alisema hiyo inatoa picha nzuri kwa Tanzania kuwa, wawekezaji wa nje wanawaamini Watanzania kufanya kazi kwa pamoja.

“Ndio maana tukipata kesi Watanzania wametapeli au kugombana na wawekezaji wa nje inatusumbua kidogo, tukizunguka huwa tunawaambia kuna Watanzania tunawatafutia uwekezaji wa ubia kupitia Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), mfano mtu analeta kiwanda cha magari au simu kama mzee Mengi (Dk. Reginald Mengi, Mwenyekiti Mtendaji wa IPP,” alisema.

Alisema miradi hiyo mpaka kipindi chake cha utekelezaji kitakapokwisha kinachoanzia miaka mitatu hadi mitano, wanatarajia itatengeneza fursa za ajira za moja kwa moja zisizopungua 115,055.

Alisema katika miradi hiyo iliyosajiliwa kwa kipindi cha miaka mitatu, miradi 478 ni ya viwanda ambavyo vimekidhi sifa za kusajiliwa TIC.

Alisema China ndiyo inayoongoza kwa kuwa na miradi 723 iliyosajiliwa TIC tangu mwaka 1990, ikifuatiwa na Uingereza na Marekani.

Habari Kubwa