Tigo yatoa msaada wa milioni 110 hospitali ya CCBRT

18Oct 2019
Kelvin Innocent
Dar es Salaam
Nipashe
Tigo yatoa msaada wa milioni 110 hospitali ya CCBRT
  • Ni katika kusaidia matibabu ya watoto wenye matatizo ya mguu kifundo (clubfoot)

KAMPUNI ya simu ya Tigo imetoa msaada wa Shilingi milioni 110 kwa Hospitali ya CCBRT kwa lengo la kusaidia uboreshaji wa huduma za afya hasa kwa wagonjwa wenye matatizo ya mguu kifundo (clubfoot) zaidi 400.

Mkurugenzi mtendaji Tigo Simon Karikari akimkabidhi mfano wa hundi ya Mil 110/- Ofisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 18,2019 katika hospitali hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tigo, Simon Karikari amesema wametoa msaada huo ikiwa ni njia ya kuongeza uelewa juu ya umuhimu wa ufuatiliaji wa mara kwa mara wa matibabu ili kuwezesha wagonjwa kupitiwa matibabu stahiki na ya wakati ili kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa hapa nchini.

“Upatikanaji wa huduma za afya kwa wagonjwa wenye ugonjwa wa mguu kifundo hasa watoto imekuwa ni changamoto kubwa hivyo tatizo hili linatakiwa kupewa kipaumbele na kwa kuona hilo Tigo tunahakikisha tunabadili historia,” amesema Karikari

Amesema kuwa kupitia msaada huo utaongeza ushiriki wa jamii na utayari wa wadau katika kuhakikisha matibabu ya uhakika kwa watoto wenye tatizo hilo yanapatikana ili kutoa fursa kwa wao kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Karikari ametoa wito kwa wadau wengine kuungana na Tigo katika kuboresha maisha ya watoto wanaozaliwa na ugonjwa wa miguu kifundo kwakuwa ugonjwa huo unaweza kutibika.

“Kupitia mchango huu tunaendele kudhihirisha dhamira yetu ya kusaidia kujenga Taifa la watu wenye afya ambao wataweza kuchangia katika shughuli za kimaendeleo na pia nitoe wito kwa wadau wengine kuungana na CCBRT ili kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii yetu,” amesema.

Naye Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi ameishukuru Tigo kuwa sehemu ya maendeleo ya hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na kuboresha maisha ya wagonjwa hasa watoto.

“Tigo imeonyesha mfano wa kazi ya sekta binafsi katika kutoa suluhisho kwa matatizo yanayozikumba jamii zetu. Kwa miaka kadhaa CCBRT imefanikiwa kutatua changamoto ya matibabu ya ugonjwa huu wa miguu kifundo kwa kuhakikisha wagonjwa wanapatiwa huduma endelevu pamoja na ufuatiliaji wa mara kwa mara,” amesema Msangi na kuongeza kuwa;

“Kupitia Tigo tumeweza kuja na mfumo wa kuwakumbusha wateja wao kwa njia ya SMS juu ya ufuatiliaji wa matibabu kwa wagonjwa ili kuhakikisha wanamaliza matibabu kikamilifu, hivyo napenda kutoa wito kwa taasisi nyingine kuunga mkono hatua hii na kwa kutambua umuhimu wa teknolojia ya meseji (SMS) katika kurahisisha mawasiliano kwa wagonjwa wake, CCBRT imeungana na Tigo na kuanzisha mfumo wa kuwakumbusha wagonjwa kufuatilia matibabu mara kwa mara.,” amesema

Ameongeza kuwa tangu ulipoanza kutumiwa mfumo huo na CCBRT, umeweza kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokatisha matibabu kabla ya wakati ambapo zaidi ya watoto 1,500 wameshanufaika na njia ya matibabu ya Ponseti (bila upasuaji) ya kutibu mguu kifundo.

Habari Kubwa