Tito adai hofu mahabusi kusongamana

02Apr 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Tito adai hofu mahabusi kusongamana

HAKIMU Mkazi Mkuu, Janeth Mtega, amemtaka Ofisa wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti na mwenzake wanaokabiliwa na tuhuma za Uhujumu Uchumi na wote walioko mahabusu kufuata mwongozo na kuchukua tahadhari ya kujikinga na virusi vya corona.

Mtega alitoa rai hiyo jana wakati akiahirisha kesi kwa njia ya mtandao kati ya ukumbi wa Mahakama ya Kisutu na Gereza la Segerea.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Hata hivyo, Tito alinyoosha mkono na alipokubaliwa alidai kuwa zuio la msongamano ni mahakamani pekee, lakini watu wanapoishi gerezani halitumiki kwa sababu wanasongamana na wao wamesongamana.

Alidai kuwa jambo ambalo linawafanya wanaishi kwa hofu, watuhumiwa wanahisi wamesahaulika na kupuuzwa katika jitihada za kitaifa za kujikinga na ugonjwa wa corona.

"Siku 14 tangu kesi yetu iahirishwe hatujawasiliana na mawakili, familia, wazazi, watoto na wake zetu, tunajisikia kutengwa katika hatua hii muhimu, tunaiomba mahakama iangalie suala hili kisheria kuona uwezekano wa kutuondoa katika ya hofu na kusahaulika," alidai Tito mbele ya Hakimu Mtega.

Akijibu hoja za utetezi, Wankyo alidai mshtakiwa ametoa hoja, lakini kutokana na kujikinga na virusi vya corona serikali ilichukua hatua mbalimbali za tahadhari na Jamhuri inawatoa hofu kuwa washtakiwa wote hawajabaguliwa bali ni tahadhari ya kitaifa kudhibiti wageni kuingia gerezani.

Hakimu alisema upande wa Jamhuri uharakishe kukamilisha upelelezi, washtakiwa wote wafuate mwongozo wa serikali kuhusu kujikinga na virusi hivyo.

Alisema washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu na kesi hiyo itatajwa Aprili 14, mwaka huu.

Mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni, Mtaalamu wa Tehama, Theodory Gyan (36), wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka matatu ikiwamo kumiliki programu ya kompyuta iliyotengezwa mahususi kufanya kosa la uhalifu na kutakatisha Sh. milioni 17.3.

Upande wa Jamhuri ulio wasomea mashtaka washtakiwa uliongozwa na Mawakili wa Serikali Wakuu, Faraja Nchimbi, Joseph Pande na Wankyo Simon.

Katika kesi ya msingi, Wankyo alidai washtakiwa wote katika tarehe tofauti kati ya Februari mosi na Desemba 17, 2019 ndani ya Jiji la Dar es Salaam na mahali tofauti nchini kwa pamoja na watu ambao hawapo mahakamani, kwa makusudi walishiriki kutenda makosa ya kiuhalifu ya kumiliki programu ya kompyuta iliyotengenezwa kufanya kosa la jinai na kuwawezesha kujipatia Sh. 17,354,535.

Nchimbi alidai katika tarehe tofauti kati ya Februari mosi na Desemba 17, 2019 ndani ya jiji na Mkoa wa Dar es Salaam kwa pamoja washtakiwa hao na wengine ambao hawapo mahakamani walimiliki programu ya kompyuta iliyotengenezwa mahususi kwa ajili ya kutenda makosa.

Mkude alidai katika shtaka la tatu, Inadaiwa kuwa kati ya Februari mosi na Desemba 17, 2019, jijini Dar es Salaam washtakiwa hao kwa pamoja walitakatisha na kujipatia Sh. 17,353,535 wakati wakijua mapato hayo yametokana na zao la kosa la kushiriki genge la uhalifu.

Hata hivyo, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi mpaka ipate kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mshataka nchini (DPP) au upelelezi utakapokamilika itahamishiwa Mahakama Kuu Divisheni ya Uhujumu Uchumi na Rushwa.

Habari Kubwa