TLP kuzunguka nchi nzima kuzungumzia miradi ya serikali

20May 2020
Dotto Lameck
Arusha
Nipashe
TLP kuzunguka nchi nzima kuzungumzia miradi ya serikali

CHAMA cha Tanzania Labour Party TLP, kimeunda timu ya kuzunguka nchi nzima kuzungumzia miradi iliyotekelezwa na Serikali ya awamu tano chini ya Dkt. John Magufuli huku kikimuhakikishia Rais Magufuli anashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao.

Katibu Mwenezi wa Taifa TLP, Godfrey Stephen.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha, Katibu Mwenezi wa Taifa wa chama hicho, Godfrey Stephen, amesema baada ya kamati kuu kumpitisha kwa kauli moja mgombea wa CCM Dkt. Magufuli kuwa ndie anafaa kugombea kwa mwaka huu katika uchaguzi mkuu na chama hicho kumuunga mkono mgombea huyo.

Stephen amesema kuwa kupitia kikosi kazi hicho watapita nchi nzima kuelezea na kumnadi mgombea huyo kwa wananchi ili wafahamu utekelezaji wa serikali yake katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli ndio maana kamati kuu ikaona anafaa kuungwa mkono na chama hicho kwa nafasi ya urais.

Aidha, Katibu huyo ameeleza kuwa chama hicho kimejipanga upya katika siasa ikiwa ni pamoja na kusimamisha wagombea nchi nzima kwa nafasi ya ubunge na udiwani kwa kuwa TLP ndio chuo cha wagombea.

“Kama unavyojua chama chetu kimezaliwa upya baada ya kufanya uchaguzi wa viongozi na Mwenyekiti wetu kuendelea kuwa Agustine Mrema hivyo sura mpya ya uongozi wa chama chetu unaakisi mageuzi makubwa kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu”amesema Stephen.

Pia amewatoa hofu wananchi wake kutokana na maamuzi ya kumpitisha mgombea wa nafasi ya Urais wa chama hicho kuwa ni Dkt. John Magufuli kutoka CCM yamefanywa na kupewa Baraka na mkutano mkuu wa chama hicho na yamekubaliwa na wajumbe wote.

Habari Kubwa