TLP yasema inaendelea  kumuunga mkono JPM

13Oct 2020
Richard Makore
MWANZA
Nipashe
TLP yasema inaendelea  kumuunga mkono JPM

CHAMA cha Tanzania Labor Party (TLP), kimeibuka na kusema kuwa bado kina nia ya kumuunga mkono mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli katika uchaguzi mkuu ujao.

Kimesema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania ilikosea kutangaza kwamba wamesitisha uamuzi huo.

Akizungumza na Nipashe, Makamu Mwenyekiti wa TLP, Domina Rwechngura, alisema msimamo wao upo pale pale wa kuendelea kumuunga mkono mgombea huyo.

“Sisi tuliishasema tangu mwezi wa tano kwamba tutamuunga mkono Rais Magufuli katika uchaguzi huu, hivyo msajili kauli yake kwamba tumesitisha uamuzi wetu hatuitambui,” alisema.

Hivi karibuni vyama vya TLP na UDP viliripotiwa kujiondoa mpango wa kumuunga mkono mgombea urais wa CCM, kutokana na kutofuata kanuni na sheria za uchaguzi.

Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, hivi karibuni alisema waliwaambia TLP na UDP suala hilo lina utaratibu ambao walitakiwa kuufuata, na walipoona hawajafuata, vyama hivyo vimekaa kimya na havisikiki tena.

Aliongeza kuwa UDP waliendelea na kazi zao za kampeni, wakiwa na mgombea wao na kutangaza sera za chama chao.

Vile vile, alisema TLP ambao waliweka mabango wameyatoa na wanaendelea na kampeni zao.

Habari Kubwa