TMA yatahadharisha upepo mkali nchini

02Jul 2020
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
TMA yatahadharisha upepo mkali nchini

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa tahadhari ya kuwapo kwa vipindi vya upepo mkali unaofika kilometa 50 kwa saa na mawimbi yatakayofikia zaidi ya mita mbili kwenye Bahari ya Hindi.

Hali hiyo inatarajiwa kutokea katika kipindi cha kuanzia Julai Mosi hadi 4.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Menaja wa Kituo Kikuu cha Utabiri cha TMA, Samwel Mbuya, maeneo yatakayoathirika na upepo huo ni mikoa ya Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Zanzibar, Mafia, Lindi na Mtwara.

Pia, alisema hali hiyo inatarajia kutokea katika maeneo yanayozunguka maziwa makuu ya Tanganyika na Nyasa katika mikoa ya Kigoma, Songwe, Mbeya na Ruvuma.

"Wananchi katika maeneo haya wanapaswa kuchukua tahadhari kwa sababu kutakuwa na athari ya kusimama kwa huduma za usafiri na kiuchumi," alisema Mbuya kwenye taarifa hiyo.

Mamlaka imewataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa ya hali ya hewa zitakazotolewa na mamlaka ili kuendelea kuchukua tahadhari.

"Mamlaka inaendelea kufuatilia kwa karibu mifumo ya hali ya hewa na tutakuwa tukitoa taarifa kwa wananchi kila wakati, lakini ni vyema pia kuanza kuchukua tahadhari mapema kila taarifa inapotolewa," alisema Mbuya.

Alisema hali inatarajiwa kutulia kuanzia Julai 5, katika maeneo ya mwambao wa Bahari ya Hindi.

Habari Kubwa