TMDA yaahidi mapambano uingizaji dawa bandia mipakani

26Nov 2020
Grace Mwakalinga
MBEYA
Nipashe
TMDA yaahidi mapambano uingizaji dawa bandia mipakani

SERIKALI  kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), imeahidi kuongeza ushirikiano na nchi jirani  katika mapambano dhidi ya uingizwaji wa dawa bandia na duni pamoja na  kukagua ubora wake.

Mratibu wa Ofisi za Kanda za  TMDA, Dk. Henry Irunde ameyasema hayo leo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wakaguzi wa dawa ngazi ya Halmashauri ambayo yaliwahusisha waganga wakuu, wafamasia na madaktari wa binadamu na mifugo kutoka halmashauri na wilaya zote za Mkoa wa Mbeya.

Irunde amesema moja ya maeneo yanayochangia uingizwaji wa dawa na vita tiba bandia ni kutokuwepo kwa ushirikiano thabiti katika kudhibiti uzalishaji na uingizwaji wa bidhaa hizo ambazo huingizwa kwa njia ya panya nchini.

“Kwa kutambua umuhimu wa ushirikiano baina ya nchi  ya Tanzania na jirani zake, TMDA sasa inakuja na mkakati wa kukaa meza moja  kujadili ni kwa namna gani wataweza kudhibiti uzalishaji na uingizwaji wa bidhaa zilizopigwa marufuku, amesema Irunde.

Amewaomba wakaguzi  57 ambao  wanaopatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wakaguzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi  kuzingatia maadili ya kazi  katika kukabiliana na vifaa tiba bandia na utoaji wa taarifa kuhusiana na bidhaa hizo.

Kaimu Meneja wa TMDA, Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Anitha Mshighati, amesema moja ya mikakati waliyoiweka ni kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika mipaka ya Tunduma na Kasumulu  ili kudhibiti uingizwaji wa dawa bandia.

Amesema kwa kuwa wakaguzi hao ni watendaji wa Halmashauri anaamini baada ya mafunzo hao watakwenda kukabiliana na kudhibiti mianya yote ilikuwa inatumika  kuingiza bidhaa zilizopigwa marufuku.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Agness Buchwa amesema uwekezaji wa viwanda vya vifaa tiba nchini utasaidia kupunguza tatizo la dawa na vitendanishi bandia nchini.

Amesema hadi sasa Mkoa wa Mbeya una jumla ya viwanda vitatu vya kutengeneza vitakasa mikono ambavyo kimsingi havikidhi mahitaji na kwamba hitaji ni ujenzi wa viwanda vya kutengeneza dawa.

Amewaomba wawekezaji kuchangamkia fursa ya uwekezaji katika dawa ili kukabiliana na tatizo ya bidhaa zilizopigwa marufuku ili kuokoa maisha ya wananchi.

Baadhi  ya  wakaguzi waliopata mafunzo hayo ni Mganga Mkuu Hospitali ya Wilaya ya Chunya, Dk. Felister Kisandu, ambaye amesema ameongeza maarifa ya kubaini mapungufu yaliyokuwa kwenye dawa hivyo atakwenda kutoa elimu kwa wananchi kuacha matumizi ya dawa ambazo zilipigwa marufuku au kumaliza muda wake.

James Mwangolombe ambaye ni Mfamasia  wilayani Kyela, amesema moja ya matatizo yanayokwambisha utendaji kazi wilayani humo ni uingizwaji  bidhaa kwa njia za panya.

Amesema mara kadhaa wamekuwa wakikabiliana  na hali hiyo na kwamba kwa sasa amejifunza mbinu za namna ya kwenda kudhibiti njia za panya lakini kuwaelimisha wananchi juu ya athari za matumizi ya bidhaa hizo.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Busokelo, Dk. Christopher Mwasongela, amesema  jamii bado  haina uelewa juu ya matumizi ya dawa zenye mwelekeo wa kulevya.

Habari Kubwa