TMDA yakamata dawa ambazo hazijasajiliwa Dar

28Jun 2022
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
TMDA yakamata dawa ambazo hazijasajiliwa Dar

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Mashariki, imekamata vifaa tiba na  dawa ambazo hazijasajiliwa zenye thamani ya Sh. milioni 294.4.

Bidhaa hizo zimekamatwa kufuatia ukaguzi maalum,  uliofanyika eneo la Mtaa wa Kitumbini katika Kata ya Mchafukoge katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza eneo la  tukio, Meneja wa Kanda wa TMDA, Adonis Bitegeko alisema; "Timu ya TMDA Kanda ya Mashariki, imefanya ukaguzi maalum katika ghala bubu kufuatia taarifa za kiintelijensia zilizofuatiliwa kwa muda mrefu.

Katika ukaguzi tuliofanya tumebaini ghala hili linalomilikiwa na Mtanzania mwenye asili ya India,"  Ramaiya Rijendra,  limehifadhi dawa mbalimbali za binadamu ambazo hazijasajiliwa kwa hiyo ubora, usalama na ufanisi wake haujulikani."

Ametaja hatua zilizochukuliwa ni kuziondoa dawa hizo baada ya kuziorodhesha.

Ameongeza kuwa,  hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa  ikiwamo kuwatoza faini isiyopungua milioni 85 na  kuziteketeza kwa gharama zao.

Ametoa wito kwa wanaoendelea kufanya biashara hizo haramu kuacha mara moja vinginevyo  watachukuliwa hatua kali  za kisheria. 

Ameendelea kuonya pia wataalamu wa dawa  wanaojihusisha na biashara hizo haramu kuwa hawatosita kuwafutia leseni zao  za kitaaluma.

Aidha, amezitaja baadhi ya dawa hizo ni pamoja na za shinikizo la damu, za kuongeza nguvu za kiume, za kutoa ujauzito na zingine nyinge.

"Rai yetu ni kwamba wale wote wanaofanya biashara haramu adhabu ni kali na hatutomuacha mtu," amesisitiza.

Ukaguzi huo ulianza jana jioni na kufanyika usiku kucha hadi lilipokamilika leo asubuhi Juni 28.

Mtuhumiwa aliyekutwa na dawa hizo alipohojiwa alikiri kuendesha ghala hilo bubu pasipo na kibali na kinyume na sheria.

Habari Kubwa