TMDA yazindua mkataba wa huduma kwa wateja

30Jun 2020
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
TMDA yazindua mkataba wa huduma kwa wateja

MAMLAKA ya Dawa na Vifa Tiba (TMDA), imezindua mkataba wa huduma kwa wateja, toleo la nne la mwaka 2020, wenye lengo la kuboresha utoaji wa huduma.

Mganga mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akifafanua jambo katika hafla ya uzindudi wa mkataba wa huduma kwa wateja wa TMDA.

Kaimu Mkurugenzi wa TMDA, Adam Fimbo, alitangaza kuanza kwa mkataba huo katika hafla ya uzinduzi uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.

Amesema mkataba huo unalenga kupunguza muda wa kusajili dawa zinazotoka nje ya nchi kutoka siku 240 hadi siku 180 za kazi.

Ameeleza pia wamepunguza muda wa usajili dawa zinazotengenezwa ndani ya nchi kutoka siku 120 hadi kufika siku 60 sawa na nusu ya muda wa awali.

Kadhalika amesema muda wa usajili wa maeneo ya biashara za bidhaa zinazodhibitiwa na TMDA umepunguzwa kutoka siku 10 hadi nane.

Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Abel Makubi (katikati) akizindua mkataba wa huduma kwa wateja, kulia Kaimu Mkurugenzi wa TMDA, Adam Fimbo.

“Pamoja na kupunguza siku za kutathmini na kusajili dawa, tumeweka pia utaratibu rahisi wa kusajili dawa ambazo zimekwisha sajiliwa kupitia Jumuiya zetu kikanda kama EAC na Sadec pamoja na Shirika la Afya Duniani(WHO)," amesema Fimbo.

Fimbo amesema hawajapunguza sana siku za kufanya uchunguzi kwenye maabara zao kutoka siku 21 hadi 20 za kazi kwa sababu taratubu za uchunguzi zinahitaji muda wa kutosha kuandaa sampuli, njia za uchunguzi, kupima vifaa na kemikali kabla ya uchunguzi.

Amesema wakati mwingine kuotesha wadudu au vimelea vya magonjwa kumesababisha kutopunguza siku ili kutoa majibu yenye usahihi na uhalisi.

Aidha amesema sababu za kuandaa mkataba huo ni kubadilika kwa majukumu ya mamlaka kutoka TFDA  na kuwa TMDA, uwekezaji mifumo ya Tehama kwa ajili ya kurahisisha huduma, msukomo katika kukuza sekta ya viwanda na hivyo sera na taratibu zimepitiwa.

Naye mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mganga Mkuu wa Serikali. Prof. Abel Makubi, akizundua mkataba huo kwa Niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Mabula Mchembe, amezikumkumbusha taasisi zote za umma kuandaa mikataba ya kurahisisha utoaji huduma nchini.

Amesema taasisi zote zinapaswa kuandaa mkataba kama wa TMDA au kitengo maalum cha huduma kwa wateja ili wanaopatiwa huduma wawasilishe kero na malalamiko yao badala ya kwenda ngazi za juu.

“Niwapongeze TMDA, kwa kuzindua mkataba huu ambao ni muongozo wa utoaji huduma wa taasisi, nizisii taasisi nyingine kufanya hivyo ndani ya miezi mitatu kama ambavyo Serikali tumeagiza,” amesema Prof. Makubi.

Habari Kubwa