Tozo zaidi zenye kero kufutwa

24May 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Tozo zaidi zenye kero kufutwa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema serikali imeanza jitihada za kufuta tozo zote ambazo zinakwamisha mazingira ya ufanyaji wa biashara zikiwamo za kwenye pembejeo.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa.

Hatua ya kufuta tozo hizo ili kuwawezesha wafanyabiashara kuzifikisha hadi ngazi ya kijiji kwa wakulima

Majaliwa alisema hayo jana bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Madaba, Kizito Mhagama, katika kipindi cha ‘Maswali  ya papo hapo  kwa Waziri Mkuu’. Mbunge huyo alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kupunguza tozo kwa maduka yanayouza pembejeo ili kumwezesha mkulima kupata pembejeo.

Waziri Mkuu alisema serikali imepokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali wakiwamo wauzaji wa pembejeo juu ya tozo mbalimbali katika uendeshaji wa shughuli zao za biashara.

"Serikali imesikia vilio vyao na sasa inafanya mapitio ya tozo hizo na itakapofikia hatua nzuri itawajulisha na kuwashirikisha kujua ni aina gani ya tozo ambayo itaondolewa au kuibadilisha ili waendelee kufanya biashara zao katika mazingira rahisi," alisema.

Kwa mujibu wa Majaliwa, kazi kubwa inayofanywa na serikali kwa sasa ni kufanya mapitio ya tozo zote kuanzia kwa wakulima hadi kwa wafanyabiashara na kutengeneza mazingira mazuri ya kufanya biashara nchini, ikiwamo ya pembejeo ili kuzifikisha kiurahisi kwa wakulima.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema kwamba tayari mawaziri wa kisekta wenye dhamana ambao wana tozo mbalimbali kwenye wizara zao zinazokwamisha ufanyaji biashara katika mazingira rafiki, wameshakutana kwa ajili ya kujadili namna ya kulipatia ufumbuzi suala hilo.

"Hata juzi nilikuwa na mawaziri hao kupata taarifa kwa pamoja kuona maeneo yote waliyoyapitia na tozo zote zinazokusudiwa kupitiwa upya na kazi hiyo ikikamilika watakutana na Kamati ya Bajeti ya Bunge, Wizara ya Fedha ili kuona namna nzuri ya kuondoa tozo hizo. Lakini baadaye suala hilo litaenda kwenye mamlaka inayotoa ridhaa ya kuondoa au kupunguza tozo,” alisema.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu alisema miradi mingi ya maji ambayo inatekelezwa kwenye maeneo mbalimbali nchini baadhi yake haitekelezwi kwa viwango vilivyokusudiwa, hivyo haiwiani na thamani halisi ya kiasi cha fedha kinachotolewa.

Hata hivyo, Waziri wa Maji wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2019/20 alieleza hatua mbalimbali zilizochukuliwa dhidi ya miradi yote ambayo haiwiani na kiasi cha fedha kilichotolewa pamoja na hatua zilizochukuliwa dhidi ya miradi yote.

Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda (CCM),  aliyetaka kujua serikali kama iko tayari kuchunguza na kuchukua hatua kwa watendaji walioshindwa kusimamia miradi ya maji na kuisababishia hasara pamoja na wananchi kukosa huduma waliyokusudiwa.

Habari Kubwa