Tozo zitakazopaa, kupungua mwakani

11Jun 2021
Romana Mallya
Dodoma
Nipashe
Tozo zitakazopaa, kupungua mwakani

SERIKALI imependekeza kufanya marekebisho katika ushuru wa bidhaa kwa kuongeza na kupunguza, ili kuongeza ufanisi.

Akiwasilisha mapendekezo ya bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha bungeni jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema marekebisho yatagusa bidhaa za bia.

Waziri huyo alisema ushuru wa bidhaa za bia zinazotengenezwa kwa kutumia shayiri iliyozalishwa Tanzania utapunguzwa kutoka Sh. 765 kwa lita za sasa hadi Sh. 620 kwa lita ili kuchochea kilimo hicho.

Alisema serikali itaanza kutoza ushuru wa bidhaa wa asilimia 10 kwenye nyuzi na kamba za plastiki zinazoingizwa kutoka nje ya nchi au kuzalishwa nchini isipokuwa zile zinazotumika kwenye uvuvi kwa lengo la kulinda mazingira na kuchochea uzalishaji na matumizi ya bidhaa za katani.

“Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya serikali kwa Sh. bilioni 2.644," alisema na kudokeza kuanzisha tozo ya ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 10 kwenye pikipiki zilizotumika kwa zaidi ya miaka mitatu zinazoingizwa nchini ili kudhibiti uingizaji wa pikipiki chakavu na kulinda mazingira na kuongeza mapato kwa Sh. milioni 263.7.

Alisema ushuru wa forodha utapunguzwa kutoka asilimia 25 hadi asilimia 10 kwa mwaka mmoja kwenye mabasi ya abiria.

Alisema wanapendekeza kupunguza ushuru wa forodha hadi asilimia 0 kutoka viwango vya awali vya asilimia 10 na asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi zinazotumika katika uzalishaji wa vifaa maalum vinavyotumika katika kupambana na ugonjwa wa corona vikiwamo barakoa, kipukusi, mashine za kusaidia kupumua na mavazi maalum ya kujikinga yanayotumiwa na madaktari na wahudumu wa afya (PPE).

Nyingine ni magunia ya katani kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwa mwaka mmoja kwenye magunia ya kitani, unga wa kakao kutoka asilimia 0 hadi asilimia 10 kwa mwaka mmoja, vifungashio vua kuhifadhia kahawa kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja na vifungashio vya kuhifadhia korosho kutoka asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja.

Waziri Mwigulu alisema serikali inapendekeza kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye simu janja za mkononi, vishikwambi na modemu ili kuhamasisha matumizi ya huduma za mawasiliano kufikia lengo la asilimia 80 ya watumiaji wa intaneti ifikapo mwaka 2025 kutoka asilimia 46 ya sasa.

"Kufuta msamaha wa VAT kwenye mikebe inayotumika kuhifadhia maziwa li kuwapunguzia gharama wazalishaji na kuchochea ukuaji wa sekta ya maziwa," alisema.

Waziri huyo alisema wanapendekeza kufuta msamaha wa kodi kwenye taa zinazotumia umeme wa jua na kutoza VAT kwa kiwango cha asilimia sifuri kwenye huduma ya usafirishaji na huduma zinazohusiana na usafirishaji wa mafuta ghafi kupitia bomba linalojengwa kwa pamoja baina ya Serikali ya Tanzania na Uganda (EACOP).

"Ninapendekeza kutoa msamaha wa VAT kwa taasisi zisizo za kiserikali (NGO) kwenye bidhaa na huduma zitakazotumika kwenye miradi inayotekelezwa na taasisi husika," alisema.

Habari Kubwa