TPA yatenga bilioni 33 ujenzi gati la kisasa

12Jun 2019
Mary Geofrey
KIGOMA
Nipashe
TPA yatenga bilioni 33 ujenzi gati la kisasa

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari (TPA), imetenga Sh. bilioni 33 kwa ajili ya ujenzi wa gati la kisasa lenye urefu wa mita 250, maghala matatu ya kuhifadhia mizigo, Ofisi ya Meneja na jengo la watumishi wa idara za Serikali katika bandari ya Kibirizi na Ujiji mkoani Kigoma.

Meneja wa Bandari ya Ziwa Tanganyika, Ajuaye Msese.

Meneja wa Bandari ya Ziwa Tanganyika, Ajuaye Msese, aliyaeleza hayo juzi kwa waandishi wa habari waliotembelea bandari hiyo kushuhudia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na TPA.

Alisema mradi huo unafanywa na Kampuni ya China Railway 15 Group Corporation, ambayo imeanza kufanya kazi tangu Februari 28, mwaka huu na umetekelezwa kwa asilimia tano.

Alisema eneo la bandari ya Kibirizi wanajenga gati hilo la kisasa ambalo litachukua zaidi ya boti 70 zinazopaki katika bandari hiyo kwa ajili ya kubeba abiria na mizigo.

“Mradi wa Kibirizi ni sehemu mojawapo ya mradi ambao una sehemu tatu, mradi wa bandari ya Kibirizi, Ujiji na mradi wa ujenzi wa ofisi ya meneja wa bandari ambao katika sehemu zote tatu utagharimu Sh. bilioni 33," alisema Msese.

Alisema katika bandari ya Kibirizi, mradi wake unagharimu takribani Sh. bilioni 20 kwa ajili ya kujenga gati hilo la kisasa na uzio wa kudhibiti watu kuingia eneo hilo kiholela.

"Pamoja na mambo mengine bandari hii itajengwa uzio wa kuzunguka eneo lote ili kudhibiti watu kuingia eneo la bandarini kiholela kwa ajili ya kufanya shughuli zao binafsi," alisema Msese.

"Kwenye mradi huu kutakuwa na uzio wa kuzunguka eneo lote la bandari na hivyo kuruhusu watu pekee wanaokwenda kwa ajili ya shughuli za bandari au wafanyabiashara na abiria lakini wengine watakuwa wanafanya shughuli zao zote nje," alisema Meneja hiyo anayesimamia bandari zote za Ziwa Tanganyika.

Miongoni mwa shughuli zisizohusiana na bandari zinazofanyika katika bandari hiyo ni watu kuchota maji na kuingia eneo hilo bila shughuli maalum.

Kadhalika alisema kabla ya kuanza kujengwa kwa gati hilo, TPA waliweka 'Floaters' zinazosaidia watu kupanda kwenye boti bila kukanyaga maji.

“Zamani watu walikuwa wakipanda na kushukia kwenye maji lakini sasa hivi tumeweka hizi ‘floaters’ ambazo zinaruhusu watu kupanda boti bila shida yoyote," alieleza Msese.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Usafiri wa Boti Bandari ya Kibirizi, Edmund Msabaha, alisema huduma katika bandari hiyo ni nzuri isipokuwa wanakabiliwa changamoto ya kutokuwa na ghala la kuhifadhia mizigo ya samaki.

“Kinachotusumbua ni kutokuwapo na ghala la kuhifadhia mizigo ya samaki  kwa sababu kwa sasa eneo linalowekwa samaki na abiria wanakaa humo humo hasa ukizingatia dagaa wana harufu mbaya," alisema Msabaha.

Getrude Filbert.

Naye abiria wa kuelekea visiwa vya jirani Getrude Filbert, alisema ujenzi wa bandari hiyo utakuwa suluhu ya kudumu kwa wakazi wa Kigoma na visiwa vya jirani.

Aidha, aliipongeza TPA kwa kuweka kivuko cha muda cha kupandia kwenye boti hali iliyowaondolea usumbufu wa kukanyaga maji.

Habari Kubwa