TPA kujenga gati kupokea meli tani 100,000

07Nov 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
TPA kujenga gati kupokea meli tani 100,000

MAMLAKA ya Bandari (TPA), inatarajia kujenga gati la kisasa lenye uwezo wa kubeba meli kubwa ya mafuta yenye ujazo wa tani 100,000.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdatus Kakoko, picha mtandao

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdatus Kakoko, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki alipotembelea Bandari ya Tanga pamoja na uongozi wa bodi hiyo, kwa lengo la kukagua mradi wa upanuzi wa kina cha maji unaoendelea katika bandari hiyo.

Alisema mpango huo ni awamu ya pili ya upanuzi wa bandari hiyo ambao tayari wameshaingia mkataba kwa ajili ya kufanya usanifu, ambao unatarajiwa kugharimu Sh. bilioni 170.

Awamu ya kwanza ya mradi ni uchimbaji wa kina cha maji kutoka mita tano hadi 17 ambao unagharimu Sh. bilioni 17 na kwamba utakapokamilika utahudumia meli kubwa zaidi.

"Kukamilika kwa miradi hii sasa kutawezesha meli kubwa ya aina yoyote duniani kutia nanga katika bandari hii ya Tanga, kuzidi zile zinazotia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam," alisema Kakoko.

Alisema kwa sasa Bandari ya Dar es Salaam ina urefu wa kina cha mita 15.5 na malengo ni kuongeza kina hicho na kufika 19.

"Kwa sasa Bandari ya Tanga ndio itakuwa na kina kirefu zaidi kuliko Dar es Salaam na Bandari hii itahudumia meli zenye ukubwa duniani," alisema Kakoko.

Alisema tayari Bandari ya Tanga imeshapokea meli kubwa ya mafuta yenye urefu wa mita 220 iliyobeba ujazo wa tani 30,000.
Kwa sasa Bandari ya Tanga ina uwezo wa kuhudumia tani 750,000 kwa mwaka na wanaendelea na mpango wa kuchukua tenda ya tani za ziada 250,000 za mizigo ya wakazi wa mikoa ya Kaskazini zinazohudumiwa na bandari za nchi jirani.

Alisema mipango mikakati ya miaka 10 ya TPA ni bandari hiyo kuhudumia tani 30,000 ifikapo 2028, wakati uwezo wa bandari zote nchini ni kuhudumia tani milioni 100.

Mwenyekiti wa Bodi ya TPA, Prof. Ignas Rubaratuka, alisema fedha zote zinazotumika katika miradi hiyo ni za ndani isipokuwa kwa Bandari ya Dar es Salaam inategemea fedha za mikopo na mchango wa serikali.

"Menejimeti ya TPA ina mpango kabambe kuhakikisha miundombinu ya bandari inaboreshwa kwa asilimia 100 ili kuhakikisha huduma zinaboreshwa na kuongeza mapato," alisema Prof. Rubaratuka.

Meneja wa Bandari ya Tanga, Ajuaye Msese, alisema kukamilika kwa miradi hiyo kutapunguza muda wa kupakua na kupakia mizigo hali itakayovutia wawekezaji wengi kutumia bandari hiyo.

"Bandari ya Tanga, itaongeza mapato yake kutokana na shughuli zitakazokuwa zinafanywa na bandari yetu," alisema Msese.

Habari Kubwa