TPA yajipanga kuongeza makusanyo

09Dec 2018
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
TPA yajipanga kuongeza makusanyo

Hatua hiyo inatokana na bandari hiyo kuwa lango kuu la kupitisha mizigo kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko.

Hatua hiyo inatokana na bandari hiyo kuwa lango kuu la kupitisha mizigo kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Aidha, katika kutimiza azma hiyo, TPA imeweka malengo ya kuzirasimisha bandari bubu zote nchini zaidi ya 250 ili kutumika kuingizia serikali mapato ambayo kwa makadirio yake yatakuwa Sh. bilioni 35 kila mwezi.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko, alisema hayo jana wakati akizungumzia utekelezaji wa miradi ya bandari na kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato.

Alisema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais John Magufuli, bandari bubu hizo zinaendelea kufanyiwa tathimini hivyo huenda zikafika 300.

“TPA tunaangalia namna tunavyoweza kukusanya mapato kupitia bandari bubu ambazo pia zinapitisha bidhaa kimagendo. Tumeanza utaratibu wa kuzirasimisha na kwa mantiki hiyo zitawezesha kukusanya mapato nusu ya yale tunayokusanya katika Bandari ya Dar es Salaam kwa mwezi," alisema.

Alisema bandari hizo zilizopo katika mikoa Pwani, Tanga, Lindi, Mtwara, Mbeya na zile za maziwa katika mikoa ya Mwanza, Kigoma na Kagera.

Kakoko alisema katika kutekeleza mikakati iliyojiwekea, bandari ya Tanga imepiga hatua kwa kuboresha miundombinu yake hali iliyosababisha kupunguza siku za kushusha mzigo kutoka siku saba hadi mbili.

Meneja wa Bandari hiyo, Percival Salama, alisema Bandari ya Tanga inatarajia kuhudumia shehena ya mizigo tani 1,267,000 kwa mwaka 2018/19 ikilinganishwa na tani 646,718 za mwaka 2016/17. Alisema bandari hiyo inaongoza kwa kutoa mizigo haraka kuliko nyingine nchini.

“Hii ni sifa ambayo tunayo peke yetu bandari ya Tanga, mteja akija na mzigo wake kama amekamilisha vibali mzigo wake unatoka ndani ya siku mbili. Mteja akija akakaa zaidi ya siku tano bila kutoa mzigo, kesho hawezi kuja tena," alisema Salama.

Alisema kuwapo kwa uharaka wa kutoa mizigo bandarini, kunapunguza gharama kwa wenye mizigo ambazo wanaingia kwa kukaa muda mrefu Bandarini.

Kutokana na kuwapo kwa urahisi huo kumewezesha meli ya tani 40,000 iliyokuwa ikihudumiwa kati ya siku sita hadi nane kwa sasa kuhudumiwa kwa siku mbili.

Salama alisema pia wamefanikiwa kurejesha wafanyabiashara walioacha kuitumia bandari hiyo ikiwemo Kampuni ya A to Z ya jijini Arusha ambayo iliacha kupitisha mzigo kupitia bandari hiyo tangu mwaka 2015.

"Bandari chakula chake ni mzigo, hivyo jitihada zetu ni kurudisha wateja waliokata tamaa kutumia bandari yetu. Huyu A to Z hivi sasa ndiye mteja wetu mkubwa na kwa mwezi anapitisha hadi kontena 91. Lakini amerudi baada ya kuboresha huduma zetu," alisema Salama.

Alisema wateja wanaangalia ubora wa huduma na kazi kubwa iliyofanyika katika bandari hiyo ni kuboresha eneo la vifaa kwa sababu shida kubwa ilikuwa kwenye mitambo iliyosababisha uondoshwaji wa mizigo kuchukua muda mrefu.

Kuhusu mapato alisema kwa mwaka 2018/2019 bandari hiyo imepangiwa kukusanya zaidi ya Sh. bilioni 25 hivyo wameweka nguvu kubwa kuboresha miundombinu na kununua mitambo ya kisasa kufanikisha malengo hayo.

Pia alisema wanatarajia kununua mitambo mipya 20 na kati ya hiyo mitano imeshawasili ikiwamo miwili ya kupakia na kushusha makontena yenye uwezo wa kubeba tani 45 kila moja.

Alisema mradi wa uboreshaji miundombinu ya bandari hiyo ulioanza kutekelezwa Desemba 3 mwaka huu, unahusisha ujenzi wa maghala ya kuhifadhia shehena yenye mita za mraba 13,000, mnara wa kuongozea meli, uwekaji sakafu na sehemu ya kupata chakula na utakamilika Machi 2020.