TPA yajivunia mapato kupaa

10Dec 2019
Elizaberth Zaya
Mwanza
Nipashe
TPA yajivunia mapato kupaa

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari (TPA), imesema inajivunia kuongezeka kwa mapato yake kutokana na mfumo na mikakati mipya ya kuongeza shehena na ufanisi katika utoaji wa huduma zake.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko, PICHA MTANDAO

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko, alisema jijini Mwanza mwishoni mwa wiki kuwa mafanikio hayo yametokana na mfumo mpya wa upimaji utendaji kazi na ukusanyaji wa mapato kwa kila bandari na kwa kila mfanyakazi.

“Mfumo huu umechangia kufanya kazi kwa ufanisi na kukusanya mapato kwa wingi na hata shehena zimezidi kuongezeka kila wakati, tofauti na ilivyokuwa katika kipindi cha nyuma,” alisema.

Alisema mwaka 2015/2016, walikuwa na ongezeko la asilimia sita hadi saba, lakini kwa sasa wamepanda hadi kufikia ongezeko la asilimia tisa hadi 11.

Kakoko pia alisema mapato yamekuwa yakipanda mwaka hadi mwaka, akibainisha kuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka jana hadi mwaka huu wamefanikiwa kukusanya Sh. bilioni 940.

"Kwa upande wa shehena tumekuwa tukipanda mwaka hadi mwaka, huko nyuma tulikuwa tukipanda kwa asilimia sita hadi saba, sasa hivi tumekwenda hadi asilimia tisa hadi 11.

"Na kwenye fedha tumekuwa tukienda hivyo hivyo, tulikuwa tukipata Sh. bilioni 300 hadi Sh. bilioni 320 kila mwaka, lakini sasa tuna ongezeko kubwa.

“Kwa hiyo baada ya kuingia menejimenti iliyopo sasa hivi na bodi, tulijiwekea malengo tukaanza kwa kuongeza mapato ya Sh. bilioni 608 (wakati wanaingia), lakini tulipoboresha mikakati zaidi, tulipanda zaidi Sh. bilioni 940, na mpaka hivi tunapozungumza, tumekwenda zaidi ya Sh. bilioni 100 kwa mara moja na mipango yetu ni kufikia Sh. trilioni 1.40," alitamba.

Pia Kakoko alikiri kwamba miaka ya 2015 na 2016 bandari ilipitia kipindi kigumu ambacho ilifikia wakati baadhi ya watu kuanza kubeza kutokana na kupungua kwa shehena na mizigo.

“Mwaka 2015/16 kilikuwa ni kipindi kigumu, kilikuwa ni kipindi ambacho baadhi ya watu walipiga picha wakisema bandari imebaki magofu, kwa hiyo tunajivunia mpango tuliouweka wa kuongeza shehena ambayo haipungui tani milioni moja kwa mwaka,” alisema.

Habari Kubwa