TPRI yatakiwa kuondoa viuatilifu vyenye madhara sokoni

18Feb 2019
Christina Mwakangale
DAR ES SALAAM
Nipashe
TPRI yatakiwa kuondoa viuatilifu vyenye madhara sokoni

ASASI ya Maendeleo na Mazingira na kudhibiti Kemikali nchini (Agenda), imeitaka Taasisi ya Kusimamia na Kudhibiti Viuatilifu Tanzania (TPRI), kuondoa viuatilifu vyenye madhara sokoni, ikiwamo kulinda ikolojia kilimo.

Afisa Progarmu Mwandamizi wa Agenda, Dorah Swai

Afisa Progarmu Mwandamizi wa Agenda, Dorah Swai aliyasema hayo jana kwenye taarifa kwa umma iliyotolewa jijini Dar es Salaam. 

Alisema kwenye utafiti uliofanywa hivi karibuni na asasi hiyo, ilibainika kuwa, viuatilifu vilivyo na madhara ni kati ya vinavyosajiliwa na taasisi hiyo iliyo chini ya Wizara ya Kilimo.

Alieleza kuwa wauzaji na watumiaji wa viuatilifu baadhi yao hawana taarifa zinazohusiana na utambuzi wa viuatilifu hivyo ikiwamo matumizi.

"Orodha ya viuatilifu hivyo vyenye madhara makubwa haijatolewa kwa wauzaji, watumiaji na jamii kwa ujumla, na hakuna mwongozo wa kuelekeza jinsi ya kuvitambua viuatilifu hivyo katika orodha ya viuatilifu vyote vilivyosajiliwa na vinavyotumika hapa nchini," alisema Swai.

Alisema viuatilifu hivyo vina madhara na  kusababisha viwango vya juu vya madhara ya papo kwa hapo, ikiwamo madhara ya muda mrefu kwenye afya na mazingira kufuatia taarifa za mfumo wa uainishaji kimataifa wa  Shirika la Afya Duniani (WHO) na Mfumo wa kimataifa wa utambuzi wa bidhaa (GHS).

"Agenda inaihimiza serikali kupitia TPRI kuandaa mpango wa kitaifa wa kuondoa viuatilifu vilivyo na madhara makubwa na kusisitiza matumizi mbadala ya viuatilifu visivyo na kemikali na kukuza kilimo ekolojia," alisema Swai.

Alisema taarifa za kimataifa zinasema madhara na vifo vitokanavyo na viuatilifu kwa kupitia mdomoni vimekadiriwa kuwa ni kwa kiasi cha vifo 186,000 na kusababisha ulemavu kwa watu 4,420,000 kwa mujibu ripoti ya Disability Adjusted LifeYears (DALYs) ya mwaka 2002.

Swai alisema kuwa watoto wana nafasi kubwa ya kudhurika na viuatilifu kuanzia mimba inapotungwa na baadhi ya njia zinazochangia kwa mtoto kuingiwa na viuatilifu ni kutoka kwa mama, kutoka kwenye mazingira ya nyumbani na ya michezoni, kula vyakula vilivyo na chembechembe za viuatilifu na ajira ya watoto. 

Habari Kubwa