TPSC yatakiwa kuwajengea uwezo watumishi wa umma

14Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
TPSC yatakiwa kuwajengea uwezo watumishi wa umma

WATUMISHI wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) wametakiwa kutoa mafunzo yatakayowajengea uwezo kiutendaji watumishi wa umma wanaopata fursa ya kujiendeleza katika chuo hicho, ili waweze kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mary Mwanjelwa, picha mtandao

Wito huo ulitolewa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mary Mwanjelwa, wakati akizungumza na watumishi wa TPSC, makao makuu na kampasi ya Dar es Salaam, wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kufahamu majukumu ya TPSC na kujiridhisha na utendaji kazi wa chuo hicho.

Mwanjelwa aliwahimiza watumishi wa TPSC kuwa wabunifu kwa kuboresha mitaala itakayowaandaa vema watumishi wa umma, sekta binafsi na wananchi wanaohitimu katika chuo hicho ili waweze kuwa na mchango katika maendeleo ya taifa.

Mwanjelwa alisema, katika ulimwengu wa sasa jamii inabadilika, uchumi unabadilika na siasa zinabadilika pia na kuwataka watumishi wa TPSC wabadilike ili utendaji wao uwe wenye kujali matokeo na wenye tija.

Aidha, Mwanjelwa, alitembelea madarasa ya kampasi ya Dar es Salaam ili kujionea vitendea kazi na kuzungumza na wanachuo ambao walimweleza kuwa, wanaridhika na elimu inayotolewa na watatumia elimu na ujuzi wanaoupata katika kulitumikia taifa.

Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu TPSC, Dk. Henry Mambo, alisema, TPSC ilianzishwa ili kusaidia zoezi la kujenga uwezo wa watumishi wa umma uwe wenye kujali matokeo katika kutoa huduma bora kwa umma na kuongeza kuwa, kwa sasa chuo kina matawi sita yaliyopo Dar es Salaam, Mtwara, Singida, Tabora, Tanga na Mbeya.

Dk. Mambo alifafanua kuwa, madhumuni makubwa ya kuanzisha chuo ilikuwa ni kuziba pengo la kukosekana kwa chuo rasmi kinachoshughulikia mafunzo ya watumishi wa umma ili waendane na mabadiliko yaliyoletwa na maboresho katika utumishi wa umma na kuongeza kuwa lengo lingine lilikuwa ni kusaidia, kukuza na kuboresha stadi za wafanyakazi, kubadili mtazamo wa utendaji wa watumishi wa umma katika suala zima la utoaji huduma bora kwa umma unaolenga kukuza uchumi na kuondoa umaskini kupitia mafunzo ya muda mfupi na mrefu.

Dk. Mambo aliainisha kuwa, tangu chuo kianzishwe mwaka 2000 kimekutoa mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi 61,221 katika nyanja ya uongozi, menejimenti na utawala.

Aidha, Dk. Mambo alisema chuo kimeruhusiwa kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa sekta nyingine ikiwamo sekta binafsi iwapo wana mahitaji ya kupata mafunzo ya kuwawezesha kuboresha utendaji kazi wao wa kila siku.

Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania ni Wakala wa Serikali iliyoanzishwa mwaka 2000 chini ya Sheria ya Wakala wa Serikali ya mwaka 1997. Kuanzishwa kwa Chuo cha Utumishi kunafuatia muungano wa Chuo cha Watumishi wa Serikali, Dar es Salaam na kilichokuwa Chuo cha Uhazili Tabora (Tabora Secretarial College).

Habari Kubwa