TPSF kutumia fursa ya SADC kusaka masoko

16Jul 2019
Beatrice Moses
Dar es Salaam
Nipashe
TPSF kutumia fursa ya SADC kusaka masoko

SEKTA binafsi wamejiandaa kutumia vyema fursa ya maadhimisho ya awamu ya nne ya Wiki ya Maonyesho ya Viwanda yanayokwenda sambamba na mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi wa Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Mkurugenzi Mtendaji wa Sekta Binafsi (TPSF), Godfrey Simbeye.

Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyekiti na mwenyeji wa mkutano huo, ambao utahudhuriwa na Wakuu wa Nchi wa Serikali kutoka nchi 16 na wanachama wa SADC, utatanguliwa na maonyesho hayo.

Akizungumza na Nipashe, Mkurugenzi Mtendaji wa Sekta Binafsi (TPSF), Godfrey Simbeye, alisema kuwa wanatarajia kuwa na washiriki 500 kutoka sekta binafsi.

“Kuna bidhaa ambazo zimepewa kipaumbele katika ushiriki wa maonyesho hayo ikiwamo dawa, saruji, plastiki na vifaa vya kilimo,” alisema Simbeye.

Alisema wanashukuru ushirikiano mzuri uliopo kati yao na serikali, kwa kuwa hata katika kamati ya maandalizi wamo wanachama kadhaa wa TPSF.

“Hatua hiyo inatia moyo nasi tumejipanga kuitumia vyema katika kuangalia masoko mapya ya bidhaa zetu zinazozalishwa nchini, ili tutanue soko kwa nchi nyingine wanachama wa SADC,” alisema.

Maonyesho hayo yamepangwa kufanyika katika ukumbi wa Mlimani City Julai 22 hadi 26, 2019, ambapo pia yatahusisha na wafanyabiashara na wajasiriamali wa nchini na wengine kutoka katika nchi wanachama.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Abdul Chacha, akizungumzia kuhusu Wiki ya Viwanda na Biashara inatokana na maazimio ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika tarehe 29 Aprili 2015 mjini Harare, Zimbabwe.

“Wiki ya Viwanda inatokana na mkakati wa viwanda ambao uliidhinishwa na wakuu wa nchi na serikali wa SADC mjini Harare, Zimbabwe,” alisema.

Akizungumza kwenye warsha ya waandishi wa habari ya kuwajengea uwezo wa kuandika habari za SADC, Chacha alisema kuwa mkakati wa viwanda wa SADC una lengo la kuongeza kasi ya kuimarisha ushirikiano na ushindani wa kiuchumi kutoka katika nchi zisizokuwa wanachama wa SADC.

Alisema mkakati wa viwanda wa SADC 2015- 2063 umegawanywa katika awamu kuu mbili; awamu ya kwanza 2015 -30 na awamu ya pili 2030-2063.

Mkakati huo umejikita katika maeneo makuu matatu ambayo aliyataja kuwa ni viwanda ushindaji na mtangamano wa kikanda na kila eneo kati ya yaliyotajwa, utekelezaji wake umependekezwa katika mpango mkakati wa viwanda wa SADC.

Awali mratibu wa vyombo vya habari kitaifa SADC, Zamaradi Kawawa Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maelezo, alisema maonyesho hayo yatafungua fursa zaidi za kibiashara.

Zamaradi aliwataka waandishi wa habari kutumia vyombo vyao kuwapasha habari wafanyabiashara, wajasiriamali na wananchi kwa ujumla kutumia nafasi hizo vyema.

Habari Kubwa