TPSF sasa yageukia maendeleo ya vijana

19Dec 2018
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
TPSF sasa yageukia maendeleo ya vijana

TAASISI ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), imesema kuna umuhimu wa kuweka mikakati mipya ili kuhakikisha vijana, ambao ni kundi kubwa nchini, wanasaidiwa kuweka mawazo yao ya biashara kwa vitendo.

Mwenyekiti wa tpsf Salum Shamte

Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Salum Shamte, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa ofisi ya Shirika la Kimataifa la Angel Investors (WBAF) ambalo limejikita kupeleka huduma za kifedha kwa vijana wasomi, wabunifu, wavumbuzi.

Shirika hilo limemteua nguli wa tasnia ya fedha Tanzania, Sabetha Mwambenja, kuwa Mkurugenzi Mkazi Tanzania. Makao makuu ya shirika hilo yako Istanbul, Uturuki.

Shamte alisema wajasiriamali wadogo na wa kati ni muhimu kutokana na ukweli kwamba idadi ya vijana nchini ni kubwa ikilinganishwa na makundi mengine.

“Kuna umuhimu wa kuweka mikakati mipya ili kuhakikisha vijana wanasaidiwa kwa ushauri kuhusu namna wanavyoweza kuyaweka mawazo yao ya biashara katika vitendo,” alisema.

Shamte alisema ufunguzi wa ofisi hiyo nchini,utawezesha sekta binafsi kufungua idara ya wafanyabiashara wadogo makao makuu yake jijini Dar es Salaam ambazo zitafanya kazi pamoja na shirika hilo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwambenja alisema shirika hilo limejikita kupeleka huduma za kifedha kwa vijana wasomi, wabunifu, wavumbuzi, wanaoanza biashara kufuatia uvumbuzi na ubunifu wao na kuwasaidia wafanyabiashara wadogo kuwa wafanyabiashara wakubwa.

“Tumeamua kujikita kulisaidia kundi hili kutokana na kubainika kuwa wametengwa na taasisi za benki huku wakishindwa kukopesheka kutokana na kushindwa vigezo ikiwemo riba kubwa,” alisema.

Alisema shirika hilo litakuwa jukwaa la kuwafikia Watanzania wabunifu, wavumbuzi wanaoanza biashara na kuwasaidia wafanyabiashara wadogo na kuwaunganisha na shirika.

“Wajibu wa shirika la Angel Investors Tanzania ni kutoa mtaji, kuwalea wahusika mpaka wafikie hatua ya kusimama wenyewe, kuwaunganisha na masoko ya huduma na bidhaa walizobuni ama kuvumbua lakini pia kuwapa taarifa zinazohusu bidhaa zao,” alisema.

Alisema tayari wameshafanya mazungumzo na sekta ya umma na binafsi ikiwamo vyuo vya elimu ya juu na ufundi kikiwamo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Alisema kwa kuanzia shirika hilo limefungua milango kwa kuwawezesha walengwa kutuma maombi kwao ili waweze kuunganishwa na WBAF, ambayo kupitia kamati yake ya uwekezaji, itayapokea maandiko ya miradi husika.

“Mpaka sasa vijana zaidi ya 500 wameshaunganishwa kupitia kiunganishi ambapo watachujwa na kufikia 66 watakaokwenda kufanya uwasilishaji katika mkutano wa mwaka wa siku tatu wa Angel Investors wa dunia,” alisema.

 

Habari Kubwa