TPSF: Tusitumie corona kupunguza wafanyakazi

25Mar 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
TPSF: Tusitumie corona kupunguza wafanyakazi

TAASISI ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), imeasa wanachama wa taasisi hiyo wasitumie ugonjwa wa corona kupunguza wafanyakazi katika viwanda au kampuni wanazozimiliki.

Mwenyekiti wa TPSF, Angelina Ngalula, PICHA MTANDAO

Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Angelina Ngalula, ndiye aliyetoa angalizo hilo alipokuwa akizungumza na wanahabari jana jijini Dar es Salaam, kwa kusema kwamba Tanzania na dunia kwa jumla zinapita katika kipindi kigumu kutokana na ugonjwa wa corona.

Hata hivyo, alisema kuwa siyo busara kutumia tatizo hilo kupunguza
wafanyakazi.

“Kupunguza wafanyakazi litakuwa ni tatizo kubwa kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Hivyo nawaomba waajiri kote nchini tushughulikie changamoto zilizopo kwa pamoja ili kulinda ajira nchini. Kutumia matatizo kujinufaisha siyo utamaduni wa Watanzania,” alisisitiza Ngalula.

Alisema kongani, mfano utalii na kilimo, ambazo zimeathirika moja kwa moja kutokana na ugonjwa wa corona zikusanywe taarifa zinazoonyesha namna mtu mmoja mmoja alivyoathirika na taarifa hizo ziwasilishwe kwenye kikosi kazi ambacho kimeshaundwa.

“Taarifa hizo zitachambuliwa na wataalamu wetu na kufikishwa serikalini. Msitengeneza makundi yenye lengo la kujinufaisha,”
alieleza Ngalula na kuongeza kwamba jambo muhimu ni kuendelea kufanya kazi kama ambavyo Rais John Magufuli amewaomba Watanzania.

“TPSF tutaendelea kuunga mkono jitihada za serikali za kufanya kazi na kuongeza tija kwa taifa, lakini lazima kuchukua hatua zinazofaa katika maeneo ya kazi ili kuwalinda wafanyakazi wasipate maambukizi ya virusi vya corona,” alisema.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Dk. Aggrey Mlimuka, alisema huu si wakati mwafaka kwa watu kufungiwa ndani kwani athari zake zitakuwa kubwa kwenye ajira na uchumi wa nchi utaporomoka.

“Zipo nchi zimefunga ofisi zote za umma na binafsi kukabiliana na ugonjwa wa corona. Sisi kama Chama cha Waajiri tunaunga mkono kauli ya Rais John Magufuli inayowataka Watanzania kuendelea kufanya kazi, huku tahadhari za kukabiliana na corona zikiendelea kuchukuliwa,’’ alisema Dk. Mlimuka na kuiomba serikali kuondoa baadhi ya tozo kwa taasisi au kampuni zitakazoathiriwa na ugonjwa wa corona.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dk. Godwill Wanga, aliwataka wafanyabiashara kuacha ubinafsi na kufikiria maslahi mapana ya nchi badala ya kutumia matatizo ya corona kujinufaisha.

“Wote tunafahamu kwamba dunia nzima inapambana na virusi vya corona. Tanzania bado hali haijawa mbaya sana na tunaomba tusiathirike zaidi,” alisema na kuongeza:

Kutumia janga la corona kupunguza ajira ni kuhatarisha uchumi wetu. Tuwe wawazi na kuelekeza changamoto zetu katika maeneo husika ili kunusuru uchumi.”

Habari Kubwa