TPSF yaainisha mambo saba muhimu miradi mikubwa

22Jun 2019
Romana Mallya
Dar es salaam
Nipashe
TPSF yaainisha mambo saba muhimu miradi mikubwa

TAASISI ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), imeainisha mambo saba muhimu kwenye miradi mikubwa ukiwamo wa Kufua Umeme wa Maji mto Rufiji huku ikizitaka kampuni za kizawa kuacha ubinafsi na badala yake ziungane katika kuitafuta kama wanavyofanya nchi nyingine.

Viongozi wa taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi pamoja na wadau wa sekta hizo wakiwa kwenye warsha iliyolenga kujadili fursa mbalimbali za kibiashara kwa kampuni za wazawa zinazotokana na mradi wa Kufua Umeme wa maji unaotekelezwa Bonde la Mto Rufiji.

Mwenyekiti wa TPSF, Salum Shamte aliyasema hayo leo katika warsha iliyoandaliwa na taasisi hiyo kujadili fursa za kibiashara kwa kampuni za ndani zinazotokana na mradi wa Maji bonde la mto Rufiji.

Katika warsha hiyo wadau wa TPSF wamepata fursa ya kupitishwa kwa undani zaidi na taasisi za serikali kuhusu fursa kwa wazawa zinazotokana na mradi huo.

Akizungumzia kwenye warsha hiyo Shamte amesema inasemekana watanzania hawatumii nguvu kubwa na ujasiri katika kutafuta kazi kwenye miradi mikubwa ikilinganishwa na kampuni za nchi za jirani.

Alitaja jambo lingine kuwa ni haki ya kila mtanzania hususan sekta binafsi kupewa taarifa za wazi namna ambavyo mkandarasi atakuwa anatoa kazi kwa kampuni za wazawa ili kusiwe na upendeleo.

"Suala la mitaji na utendaji kazi ni changamoto kubwa inayoondoa kampuni za wazawa kwenye ushindani, inabidi hili liangaliwe kwa jicho la uwekezaji ikibidi kuanzisha mpango wa kutoa dhamana ya serikali au kuwe na mfumo maalum wa kuwezesha dhamana hiyo kupatikana," amesema.

Shamte amesema uwajibikaji, umahiri, nidhamu, uaminifu wa kampuni za wazawa wakati wanapopata fursa kushiriki katika miradi mikubwa ni muhimu kwa sababu kumekuwa na malalamiko ya utendaji usioridhisha kwa baadhi yao.

Mhandisi Edward Ishengoma kutoka Wizara ya Nishati, aliyemwakilisha Waziri wa wizara hiyo, Dk. Medard Kalemani, alizitaka kampuni za kizawa zitakazopata fursa kwenye mradi huo zihakikishe zinatoa huduma nzuri zenye kuridhisha.

Alisema mradi huo ambao utatekelezwa kwa miaka mitatu unatarajia kutoa ajira kwa watu 6000 ambapo fursa zilizopo kwa wazawa ni huduma mbalimbali za kibidamu ikiwemo chakula, sehemu za kulala na vifaa vya ujenzi.

Mratibu wa mradi huo wa Mto Rufiji, Justus Mtolera, akizungumzia kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme (Tanesco), Dk. Tito Mwinuka, alizitaka kampuni za wazawa zihakikishe kuwa zipo vizuri kivifaa, ziwe na wafanyakazi wa kutosha na ziwe zimesajiliwa.

Katibu Mtendaji wa Baraza la taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Bang'i Issa aliwakumbusha wazalishaji wa ndani ambao watanufaika na mradi huo kuwa ubora na bei za bidhaa na vifaa watakavyozalisha ni muhimu.

Habari Kubwa