TPSF yawaunganisha  Watanzania, Waturuki

23Feb 2018
Romana Mallya
Nipashe
TPSF yawaunganisha  Watanzania, Waturuki

TAASISI ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), imewataka wafanyabiashara wazawa kuchangamkia fursa ya kushirikiana na wafanyabishara wa Uturuki waliowekeza kwenye sekta ya kilimo.

Mkurugenzi wa Huduma kwa Wanachama wa TPSF, Louis Accaro

Imesema ushirikiano na wenzao wa Uturuki, utasaidia kuinua sekta hiyo nchini ikiwa ni pamoja na kujenga viwanda vya kuzalisha mashine.

Mkurugenzi wa Huduma kwa Wanachama wa TPSF, Louis Accaro, alitoa wito huo jana jijini Dar es Salaam, baada ya kukutana na ujumbe wa wafanyabiashara wanaoshughulika na uuzaji usambazaji na utengenezaji wa mashine za kilimo waliokuja nchini kutafuta fursa hiyo.

Wafanyabiashara hao ambao wako nchini kwa siku tatu tangu juzi, wamekuja kupitia chama chao  kijulikanacho kama 'Central Anatolian Exporters' kilichoko jimbo la Anatolian, Uturuki.

Accaro alisema ujumbe huo umekuja mahsusi kwa maeneo matatu ambayo ni kupata wabia wanaoweza kushirikiana nao kuuza bidhaa wanazozalisha pamoja na kushirikiana na wafanyabiashara Watanzania katika kukuza teknolojia ya kilimo na kwamba wako tayari kujenga viwanda vya kuzalisha mashine za kilimo.

Accaro alisema Watanzania ambao wako tayari kushirikiana nao waende ofisi za TPSF au Ubalozi wa Uturuki nchini.

"Rais wao alishakuja Tanzania na kukutana na Rais John Magufuli na makubaliano yaliyopo ni ujenzi wa reli ya Standard Gauge na ndege za Uturuki kila siku zitakuwa zinakuja Tanzania, " alisema Accaro.

Aidha, alisema ushirikiano na Uturuki ni muhimu kwa kuwa wenzetu wamepiga hatua kwenye sekta ya kilimo wana mashine bora na za kisasa na ikilinganishwa na maeneo mengine bei zao ni rahisi.

Accaro alisema ujio wa wafanyabiashara hao ni muda mwafaka kwa sababu Tanzania inatekeleza azma ya ujengwaji wa viwanda ambavyo vitawezesha kufikia uchumi wa viwanda.

Pia alisema Uturuki imepiga hatua kwenye soko la chakula barani Ulaya hivyo Tanzania ikishirikiana nao itakuwa rahisi.

Katibu Mkuu wa chama cha wafanyabiashara hao kutoka Uturuki, Ozkan Aydin, alisema umuhimu wa ziara hiyo ni kuchangia katika sekta ya kilimo na kuangalia uwezekano wa fursa ambazo watashirikiana katika nyanja ya kilimo baina ya nchi hizo mbili.

 Alisema lengo lingine ya ziara hiyo ni kuwapa taarifa wafanyabiashara wa Uturuki kuhusu fursa za kilimo zinazopatikana nchini Tanzania ili waje kuwekeza.